Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuipa kisogo Bucha ilikuwa ngumu lakini sikuwa na budi:Mkimbizi Yuliia

Uharibifu katika jengo la makazi Bucha, Kyiv, Ukraine.
© Said Ismagilov
Uharibifu katika jengo la makazi Bucha, Kyiv, Ukraine.

Kuipa kisogo Bucha ilikuwa ngumu lakini sikuwa na budi:Mkimbizi Yuliia

Amani na Usalama

Bucha mji ambao wakati mmoja ulikuwa mji wa bweni tulivu karibu na Kyiv, sasa ni sawa na uwanja wa mauaji ya halaiki ya raia katika vita vinavyozidi kuwa vya kikatili nchini Ukraine. 

Mkimbizi Yuliia anatoka huko. Wiki sita zilizopita, maisha yalikuwa rahisi kwake yeye na mumewe Valerii, na mtoto wao mdogo Artemko, walikuwa wamehamia kwenye nyumba mpya katika eneo lenye utulivu, lililotawaliwa na uoto wa kijani. Alikuwa na kazi ya kutengeneza nywele saluni na hakuna chochote alichikipenda zaidi ya wakati mteja anapoondoka kwenye saluni yake akiwa mrembo na mwenye ujasiri. 

Kila kitu kilibadilika asubuhi moja ya kutisha mwishoni mwa mwezi wa Februari. Vita, vurugu, sauti kubwa na ya kutisha ilipiga kelele kutoka upandfe wa kaskazini. Huku mtaa wake ukiwaka moto, Yuliia hakuwa na budi bali kuamua kutoroka. 

Yeye na familia yake, akiwemo mama yake Zinaida, walijiunga na wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 7.1 (IDPs) katika nchi kubwa zaidi ya Uropa (kuanzia tarehe 1 Aprili 2022).  

Baada ya majuma manne wakiwa njiani, walifika katika jimbo la magharibi la Zakarpattia, mamia ya kilomita kutoka mji wa nyumbani kwake uliosambaratika. 

Mama aliyekimbia Bucha na familia yake akiwa na mwanae katika kambi ya Zakarpattia, Ukraine.
© IOM/Jana Wyzinska
Mama aliyekimbia Bucha na familia yake akiwa na mwanae katika kambi ya Zakarpattia, Ukraine.

Yuliia alipoona picha na video za kutisha za mauaji na uharibifu huko Bucha, mara moja alibubujikwa na machozi na kubaki mdomo wazi kwa muda.  

"Kiwango hiki cha machafuko na ukatili hakiwezekani kueleweka," alisema. "Hilo sio jambo ambalo ungetamani limtokee mtu hata kama ni adui, lakini ni jambo ambalo halitasamehewa wala kusahaulika." 

Kutoka kwa majirani zake, Yuliia alipata habari kwamba baada ya familia yake kuondoka, gorofa yao ilivamiwa na kuchukuliwa na mali zao kuporwa.  

Kiwanda ambacho mama ya Yuliia alifanya kazi kiliharibiwa na mabomu. Ingawa mamlaka ya Ukraine imepata udhibiti tena wa eneo hilo, watu bado hawaruhusiwi kurejea nyumbani kutokana na hatari za mabomu ya kutegwa ardhini , na mabaki mengine ya vifaa vya milipuko ya vita. 

Wafanyakazi wa IOM wakiwa kwenye shule kijiji cha Bushtyno ambapo misaada kwa ajili ya wakimbizi wa ndani.
© IOM/Jana Wyzinska
Wafanyakazi wa IOM wakiwa kwenye shule kijiji cha Bushtyno ambapo misaada kwa ajili ya wakimbizi wa ndani.

Hapa Zakarpattia, hatimaye wanaweza kupata mapumziko. Pamoja na mamia ya wakimbizi wengine wa ndani au IDPs, na walipata makazi ya muda katika shule iliyo katika mji mdogo wa Bushtyno.  

Wafanyakazi wa kujitolea kutoka Ujerumani, Polandi na Jamhuri ya Czech wamejitahidi kadiri wawezavyo kubadilisha vymba vya madarasa kuwa vyumba vizuri vya kulala. Ukumbi wa michezo umekuwa ghala kuu la mahitaji yote ya maisha ya kila siku. 

“Kwa hiyo tupo hapa. Hii ndio nyumba yetu sasa. Tuna kila kitu tunachohitaji, na watu wema wanatusaidia kwa kila njia,” anasema Yuliia. “Ingawa tunalala kwenye magodoro sakafuni sasa, makombora hayarushwi juu ya vichwa vyetu na mtoto wangu yuko salama. Hili ndilo jambo pekee ambalo ni muhimu sasa." 

Tanki iliyoharibiwa Bucha, katika vitongoji vya Kyiv, Ukraine.
© Marian Prysiazhniuk
Tanki iliyoharibiwa Bucha, katika vitongoji vya Kyiv, Ukraine.

 

Anatumaini kwamba mwanawe hatakuwa na kumbukumbu zozote za wiki hizo za kutisha za hofu na kufungasha virago kukimbia.  

"Hatuna mali nyingi za kibinafsi lakini kinachovunja moyo wangu ni kwamba hatukuweza kumchukulia Artemko vitu vyake vyovyote vya kuchezea . Anapenda magari na, nyumbani, alikuwa na vitu vingi vya kuchezea vya gari, ambavyo anavikosa sana na anauliza kila wakati ni lini anaweza kurudi nyumbani kucheza navyo tena. Nataka awe mtoto tu, acheze michezo na atumie wakati na watoto wengine. Ikiwa angeweza kuwa na vifaa vya kuchezea au baiskeli, angefurahi sana. Na ingenifurahisha pia.” 

Vitu vya kuchezea, na hata baiskeli vinaweza kuwa rahisi kupatikana, na kuleta tabasamu kwa mama na mtoto. Lakini hivi sasa, wamekwama, hawana nyumba, hawana kazi, hawajui jinsi gani ya kuendelea na maisha. 

 

Makaburi ya halaiki Bucha, Ukraine.
© Marian Prysiazhniuk
Makaburi ya halaiki Bucha, Ukraine.

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limekuwa ikitoa msaada muhimu wa kibinadamu kwa watu waliokimbia makazi yao kama Yuliia na familia yake. Hatua inazochukuliwa na IOM zinajumuisha msaada wa chakula, vitu visivyo vya chakula na usafi, pesa taslimu, huduma yam afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, pamoja na kuzuia biashara haramu ya binadamu na ukatili na unyanyasaji wa kingono.  

Zaidi ya watu 50,000 wamepokea msaada wa kibinadamu kutoka kwa IOM nchini Ukraine tangu kuanza kwa vita.