Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Thamani ya mchango wa wanawake haielezeki, bila ujumuishwaji wao hakuna maendeleo:UN

Habari za Un zinazungumzia habari za mchango wa wanawake kutoka kote duniani katika siku hii ya wanawake duniani
UN News
Habari za Un zinazungumzia habari za mchango wa wanawake kutoka kote duniani katika siku hii ya wanawake duniani

Thamani ya mchango wa wanawake haielezeki, bila ujumuishwaji wao hakuna maendeleo:UN

Wanawake

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake hii leo Umoja wa Mataifa umehimiza kuthamini mchango wao na kuwajumuisha katika kila nyanja ili kutimiza ajenda ya maendeleo endelevu na kukabili changamoto zingine zikiwemo janga la COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Sima Bahous pamoja na mchango wao mkubwa wanawake kote duniani wanaendelea kukabiliwa na changamoto lukuki matahalani hivi sasa nchini Ukraine inashuhudiwa hali ya kuogofya ambako athari za vita kwa wanawake na wasichana wakiwemo maelfu ya watu waliotawanywa ni kumbusho kwetu sote kwamba “Vita vyote kuanzia Ukraine hadi Myanmar, mpaka Afghanistan , kuanzia Sahel hadi Yemen wanawake na wasichana ndio wanaolipa gharama kubwa” na hivyo kusisitiza wito wa Katibu mkuu wa kutaka vita vikome mara moja. 

Mbali ya vita Bi. Bahous amekumbusha kwamba janga la coronavirus">COVID-19 limezidisha pengo la usawa na kuwatumbukiza mamilioni ya wanawake na wasichana katika umasikini mkubwahuku likirejesha nyuma hatua zilizopigwa katika ajira, afya na elimu. 

Pia ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi nayo amezidisha mara dufu tishio lakini “Wanawake na hasa wasichana wana suluhu ya changamoto hiyo. Tunayo fursa ya kuwaweka wanawake na wasichana katika kitovu cha mipango na hatua tukijumuisha suala la mtazamo wa kijinsia katika sera na sheria za kitaifa na kimataifa.” 

Hivyo katika siku hii amesisitiza kuwa wanawake sio tu wana majibu ya lengo namba 5 la maendeleo endelevu lakini kupitia kusongesha usawa wa kijinsia wana majibu ya malengo yote 17 ya ajenda ya maendele. 

Wanawake walinda amani wanaohudumu katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMIS
UN Photo/Gregorio Cunha
Wanawake walinda amani wanaohudumu katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMIS

Wakati wa kumuinua mwanamke ni sasa

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake amesisitiza kuwa pamoja na mchango wao mkubwa katika kila nyanja ya maisha fadhila wanazolipwa ni kidogo sana hali ambayo amesema inapaswa kubadilika kuanzia sasa 

“Kuanzia sasa kwenye siku hii ya kimataifa ya wanawake , ni wakati wa kusongesha mbele mshale wa saa, kwa kila mwanamke na msichana , kupitia hakikisho la elimu bora kwa kila msichana ili waweze kujenga maisha wayatakayo na kuifanya dunia kuwa mahala bora kwetu sote. Kupitia uwekezahi wa mafunzo kwa wanawake na ajira zenye staha. Kupitia hatua madhubuti kutokomeza ukatili wa kijinsia, kupitia hatua mujarabu za kuilinda sayari yetu na kupitia huduma kwa wote ambayo inaenda sanjari na mifumo ya ulinzi wa kijamii. Ukosefu wa usawa wa kijinsia kimsingi ni suala la mamlaka, katika ulimwengu unaotawaliwa na wanaume na utamaduni unaotawaliwa na wanaume. Mahusiano haya ya mamlaka lazima yabadilishwe.” 

Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Catherine Russel akiongeza sauti yake amesema “Siku hii tunatambua mafanikio yaliyopiganiwa sana na jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya wanawake na wasichana duniani, na tunaongeza ahadi yetu ya kupanua wigo wa faida hizo kwa kila msichana, kila mahali. Lakini vita vya usawa wa kijinsia bado viko mbali sana. Hatuwezi kuruhusu kizazi cha wasichana kubeba gharama ya janga hili kwa maisha yao yote. Tunapofanya kazi kujikwamua na janga la COVID-19 , wasichana lazima wawe kitovu cha mwitikio wa janga hili kimataifa, kitaifa, na na katika mipango ya kujikwamua.” 

 Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa asilimia 70 ya wafanyakazi wote wa afya ni wanawake. 

Wanawake ndio hufanya kazi ya matunzo ya bila malipo mara tatu zaidi ya wanaume 

Kwa mantiki hiyo Umoja wa Mataifa unasema “Kwa kiwango hiki, usawa wa kijinsia katika nafasi za juu utachukua miaka 130 kufikiwa.”