Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama limepiga kura kuitisha kikao maalum cha Baraza Kuu kuhusu hali ya Ukraine

Wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Baraza la Usalama limepiga kura kuitisha kikao maalum cha Baraza Kuu kuhusu hali ya Ukraine

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kwa dharura leo mjini New York Marekani kupiga kura ya azimio la kuitisha kikao maalum cha  nadra cha wajumbe wote 193 wa Baraza Kuu kuhusu uvamisi wa Uriusi nchini Ukraine.

Kura ya leo kwenye Baraza la Usalama lenye wanachama 15 ni ya kitaratibu hivyo hakuna hata mmoja kati ya wajumbe watano wa kudumu wa Baraza hilo ambao ni Urusi, Uchina, Ufaransa, Uingereza na Marekani anayeweza kutumia kura yake ya turufu. Hatua hiyo inahitaji kura tisa za ndio ili kupitishwa.

Kura ya kuitisha kikao cha Baraza Kuu

Na mara baada ya Rais wa Baraza hilo ambaye ni Urusi kwa mwezi huu ajenda ikapitisha na kura ikapigwa. Na matokeo ya kura hiyo ni kwamba azimio limepitishwa la kulitaka Baraza Kuu kuitisha kikao maalum kujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

Kura hiyo imepitishwa baada ya wajumbe 11 kupiga kura ya ndio. Mjumbe mmoja ambaye ni Urusi kura ya hapana na wajumbe watatu ambao ni China, India na Emarati (UAE) wamejizuia kupiga kura. 

Mswada wa azimio hilo umepewa namba 2623-2022.

Baraza la Usalama lakutana kujadili hali ya Ukraine
UN Photo/Evan Schneider
Baraza la Usalama lakutana kujadili hali ya Ukraine

Kikao cha Baraza Kuu

Kupitishwa kwa mswada huo wa azimio kutafanya Baraza Kuu kukutaka kwa kikao hicho maalum cha dharura kwa mara ya 11 tangu mwaka 1950.

Kikao hicho cha Baraza Kuu kitafanyika chini ya azimio la “Mshikamano kwa ajili ya amani “azimio ambalo linasema kwamba katika hali ambayo Baraza la Usalama limeshindwa kuchukua hatua kwa sababu ya kutoungwa mkono na wajumbe wote 5 wa kudumu ambao wana kura ya turufu ili kudumisha amani na usalama wa kimataifa , Baraza Kuu litajadili suala hilo mara moja huenda likatoa mapendekezo kwa nchi wanachama kwa ajili ya kuchukua hatua za pamoja ikiwemo matumizi ya vikosi vya kijeshi endapo ni lazima ili kudumisha na kurejesha amani na usalama wa kimataifa.

Azimio hilo 377A lilipitishwa tarehe 3 Novemba 1950 baada ya mjadala wa siku 14 za mjadala wa Baraza kuu na kupigiwa kura na wajumbe 59 wa wakati huo ambapo lilipita kwa kura 52 za ndio, 5 za hapana na mjumbe mmoja hakupiga kura.

Kwa mujibu wa azimio hilo kikao maalumu kinapaswa kufanyika ndani ya saa 24 tangu Baraza la Usalama kupitisha mswada wa azimio wa kuomba kikao hicho.