Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wa Lebanon 'wanastahili ukweli' – Katibu Mkuu wa UN ziarani Lebanon 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (katikati) akiweka shada la maua kuwaenzi waathirika wa mlipuko wa mwaka 2020 katika Bandari ya Beirut, Lebanon ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 200.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (katikati) akiweka shada la maua kuwaenzi waathirika wa mlipuko wa mwaka 2020 katika Bandari ya Beirut, Lebanon ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Watu wa Lebanon 'wanastahili ukweli' – Katibu Mkuu wa UN ziarani Lebanon 

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika siku yake ya pili ziarani Lebanon amezuru eneo la bandari ya Beirut ambako mnamo mwaka jana mwezi Agosti kulitokea milipuko na kusababisha madhara makubwa kwa mali, mazingira na watu.  

Akiwa katika eneo hilo la bandari ameweka shada la maua kwenye eneo la kumbukumbu ya waathirika wa mlipuko huo ambao uliacha uharibifu mkubwa hadi kufikia hatua iliyoitwa "Beirut-shima" ikifananishwa na kile kilichotokea Hiroshima Japan baada ya mlipuko wa nyuklia mnamo mwaka 1945. 

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Bwana Guteres amerejelea kile alichokuwa amewaeleza wanahabari akisema akisema anatoa pole kwa waathirika wa mlipuko huo mbaya wa mwaka jana katika Bandari ya Beirut ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 200 akisisitiza kwamba, “uchunguzi usio na upendeleo na wa wazi kuhusu tukio hili la kutisha ni muhimu kuhakikisha haki inatendeka." 

Tweet URL

 

Akizungumza na waandishi wa habari hapo hapo katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Katibu Mkuu Guterres amezungumzia kuhusu ziara yake katika Bandari hiyo, akisema ni wakati wa hisia sana, "mateso ya watu, kwanza kabisa, wale walioangamia, familia zao, waliojeruhiwa, athari kubwa."  

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba amekuwa akipokea ujumbe kutoka kwa waathirika wengi wakidai, "haja ya ukweli kuwekwa wazi, kwa hitaji la uchunguzi huru ambao unaweza kutoa ukweli huo." 

Guterres amesema anaelewa vyema kero zao na anatumai taasisi zitaweza kuwahakikishia hilo. 

Kwa mujibu wa wataalamu wa tetemeko la ardhi, nguvu ya mlipuko huo uliotokea katika bandari ya Beirut, ni sawa na tetemeko la ardhi la ukubwa wa 3.3 katika kipimo cha Richter (vipimo vinavyotumika kupima tetemeko la ardhi). 

Mlipuko mkubwa 

Ulikuwa ni mlipuko mkubwa uliotokea katika hatua mbili katika mwaka huo wa 2020. Mlipuko wa kwanza ulitokea saa 6:08 mchana kwa saa za huko tarehe 4 mwezi wa Agosti, baada ya moto kuzuka katika moja ya maghala yaliyokuwa na kiasi kikubwa cha madini ya ammoniamu, na kufuatiwa na mlipuko mkubwa uliosababisha uharibifu mkubwa katika bandari hiyo. Sehemu kubwa za mji mkuu, Beirut, pia ziliathiriwa. 

Mlipuko huo uliua takribani watu 217, kujeruhi zaidi ya watu 6,000, kuzifurusha familia zipatazo 300,000 kutoka katika nyumba zao zilizoharibiwa, na kusababisha uharibifu mkubwa na hasara inayokadiriwa kuwa mabilioni ya dola. 

Wakimbizi wa Kipalestina wana hofu ya kusahaulika 

Licha ya hali ya hewa ya mvua, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezuru katika mji wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon, ambako ametembelea ‘Shule ya Mchanganyiko ya Lydda’ inayoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA. 

Tweet URL

 

Usiku wa kuamkia zaiara ya Bwana Guterres, UN News ilikuwa imemhoji Afisa Habari wa UNRWA Bwana Fadi Al-Tayyarr katika shule hiyo na kumuuliza kuhusu umuhimu wa umuhimu wa ziara hii kwa wakimbizi wa kipalestina akasema ziara hiyo inakuja wakati wa mazingira magumu kwa Lebanon na kwa wakimbizi wa Kipalestina, hivyo ni muhimu kwani, "wakimbizi wa Kipalestina wana hofu kwamba watasahauliwa, na kwamba watatengwa." 

Kwake, ziara hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni, “utambuzi wa wazi kwamba wakimbizi hawa bado wapo, na kwamba Umoja wa Mataifa unawachukulia kuwa tatizo lao bado lipo. Kwa hiyo, ni lazima tuchukue hatua. Sote tunapaswa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili, na ujio wake katika shule hii na uwepo wake na kukutana na wanafunzi hawa pia ni ujumbe katika muktadha huo huo, na hakuna shaka kwamba hii itakuwa fursa kwao kujieleza wanachohisi, matatizo yao, na mahangaiko yao kwa mkuu wa shirika hili la kimataifa.” 

Kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi 

Aidha katika ziara yake hii, Katibu Mkuu Guterres pia amekutana leo na viongozi wa Lebanon, akiwemo Spika wa Bunge, Nabih Berri, na Waziri Mkuu, Najib Mikati. 

Tweet URL

 

Katika mkutano na waandishi wa habari kufuatia mikutano hiyo, Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake, akisema kuwa kuna, "uhakikisho wa wazi kwamba uchaguzi utafanyika mwanzoni mwa mwezi Mei kabla ya tarehe ya kikatiba kutajwa na hii ina maana kwamba Lebanon itaweka hali ya kutengeneza upya Bunge lake na kwa hilo, bila shaka, kuweka utulivu mpya wa kisiasa kwa siku zijazo."