Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimeshtushwa na serikali ya Ethiopia kutimua maafisa wa UN:Guterres 

Mfanyakazi wa WFP akisaidia usambazaji wa chakula kaskazini mwa Ethiopia
© WFP/Claire Nevill
Mfanyakazi wa WFP akisaidia usambazaji wa chakula kaskazini mwa Ethiopia

Nimeshtushwa na serikali ya Ethiopia kutimua maafisa wa UN:Guterres 

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa sana na kitendo cha serikali ya Ethiopia kuwafurusha maafisa wa Umoja wa Mataifa nchini humo. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani hii leo Guterres amesema, “nilishtushwa na habari kwamba Serikali ya Ethiopia imetangaza maafisa saba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na maafisa wakuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa,  kama watu wasiokubalika au kutakikana nchini humo  au persona non grata.” 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba shughuli zote za kibinadamu za Umoja wa Mataifa zinaongozwa na kanuni kuu za ubinadamu, kutopendelea, na uhuru. 

Kwa mujibu wa duru za Habari maafisa hao saba wamepewa saa 24 kuondoka nchini humo na wanashutumiwa kuingilia sera za ndani za nchi. 

Nchini Ethiopia, Umoja wa Mataifa unatoa msaada wa kuokoa maisha ukiwa ni pamoja na chakula, dawa, maji, na vifaa vya usafi  kwa watu wanaohitaji sana msaada huo.  

Katibu Mkuu ameongeza kuwa, “nina imani kamili na wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa ambao wako nchini Ethiopia wakifanya kazi hii. Umoja wa Mataifa umejizatiti kuwasaidia watu wa Ethiopia ambao wanategemea msaada wa kibinadamu. Na sasa tunajadiliana na serikali ya Ethiopia kwa matarajio kwamba wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliotimuliwa wataruhusiwa kuendfelea na kazi yao muhimu.”