Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya UNIDO yainua maisha ya wavuvi Sudan Kusini

Uvuvi ni fursa ya upatikanaji wa chakula na ajira kwa watu wengi duniani
UN Photo/Martine Perret
Uvuvi ni fursa ya upatikanaji wa chakula na ajira kwa watu wengi duniani

Mafunzo ya UNIDO yainua maisha ya wavuvi Sudan Kusini

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuwaondoa watu kwenye umasikini ni lengo la kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ya Umoja wa Mataifa, ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda UNIDO limeanza kuona matokeo chanya kwa wavuvi kupitia mafunzo wanayotoa kwa vikundi mbalimbali vya uvuvi nchini Sudan Kusini. 

Video ya UNIDO imeonesha wavuvi wakiwa ndani ya mtumbi wakisaka samaki katika mto Nile nchini Sudan kusini, lakini vifaa hivi vya uvuvi ni duni na ndio maana UNIDO kwakushirikiana na Serikali ya CANADA wameendesha mafunzo ya kuboresha mnyororo mzima wa uvuvi mpaka samaki kuwafikia walaji wa mwisho.

Mafunzo hayo yanagusa mnyororo mzima wa uvuaji samaki, kuongeza safari za kwenda kuvua samaki, usindikaji bora kwakutumia moshi, usalama wa wavuvi, utengenezaji bora wa aina mbalimbali wa samaki ili kuwavutia wanunuzi na usafirishaji bora kutoka katika kambi za uvuvi kupeleka mjini Kama Juba kwa wateja wenye kuweza kununua kwa bei zenye kuwapa faida zaidi wavuvi.

Adil al Nor ni mmoja wa wavuvi zaidi ya 1,200 wanaonufaika na mafunzo hayo “Mafunzo niliyopewa na UNIDO yamenisaidia sana, nimejifunza jinsi ya kutunza samaki baada ya kuwavua, na kuongeza faida yangu kwenye uuzaji wa samaki. Nimejifunza vitu vingi vya maana kwenye kozi zinazotolewa na UNIDO” 

Mshauri mkuu wa kiufundi wa UNIDO Laraisse Esserrhini anasema wanatoa mafunzo lakini pia nao wanajifunza kutoka kwa wavuvi, “Uwekezaji mkubwa upo kwenye mafunzo, kwahiyo teknolojia yoyote tunayotaka kuianzisha tunaifanya iwe rahisi kupokelewa, hatahivyo tunaenda sambamba na wapokeaji na watumiaji wa teknolojia hiyo ili kuielewa, kuikubali na kuitekeleza”