Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mfuko wa usaidizi wa dharura wa UN, CERF umesaidia kusambaza misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwemo chakula kama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako mgogoro usiomalizika umeacha wananchi bila mahitaij  ya kimsingi

Dola Milioni 135 zatolewa na UN kusaidia wanaokabiliwa na Njaa

MINUSCA/Nektarios Markogiannis
Mfuko wa usaidizi wa dharura wa UN, CERF umesaidia kusambaza misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwemo chakula kama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako mgogoro usiomalizika umeacha wananchi bila mahitaij ya kimsingi

Dola Milioni 135 zatolewa na UN kusaidia wanaokabiliwa na Njaa

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 135 kutoka kwenye Mfuko wake wa dharura (CERF) ili kuongezea kwenye shughuli za kibinaadamu katika nchi 12 barani Afrika, Amerika na Mashariki ya Kati, amesema Mratibu wa Mfuko huo Bwana Mark Lowcock akiwa mjini New York, Marekani.



 

Amesema fedha hizo zimetolewa kufuatia takwimu zilizotolewa wiki iliyopita, zikionesha zaidi ya watu 350,000 wanakabiliwa na njaa  katika mji wa Tigray Ethiopia, na tishio la njaa katika nchi ya Burkina Faso, Kusini mwa Madagascar, kaskasini- Mashariki mwa Nigeria, Sudan Kusini na Yemen.
Mark Lowcock ameongeza kuwa “Njaa inaendelea kuongezeka maeneo kadhaa hivi sasa, mgawanyo huu wa fedha zilizotolewa unaweza kuleta tofauti kati ya maisha na kifo, kwa mamilioni ya watu wanaotegemea msaada ili kuishi. Msaada utatoa vitu muhimu kama maji safi, malazi na chakula kwa watu walio na uhitaji sana wakati huu.”
Ameeleza fedha hizo zitagawanywa kwenye mashirika ya misaada kama ifuatavyo, Syria itapata dola milioni 20, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo -DRC dola milioni 20, Ethiopia zilielekezwa mkoa wa Tigray Dola milioni 13.
Nchi za Afghanistan, Nigeria na Sudan Kusini kila moja itapata dola milioni 11 kusaidia shughuli za misaada. Na fedha zilizosalia zitapelekwa Madagascar dola milioni 8, Venezuelea dola milioni 7, Chad dola Milioni 7, Burkina Faso dola Milioni 7, Cameroon dola Milioni 5, na Msumbiji dola milioni 5. Miradi ya kusaidia watu wenye ulemavu imetengewa dola milioni 10. 
“Mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuzidi misaada ya kibinadamu inayotolewa, na sio mizozo yote inayopewa uangalifu sawa wa uhitaji wa kifedha, na ndio maana mfuko huu kwa sasa ni muhimu kupita wakati mwingine wowote sababu unakuwa nyenzo muhimu ya kurekebisha usawa kwa kuhakikisha kuwa kazi muhimu ya misaada inaendelea kila mahali.” Amesema Lockcock. 
Tangu kuanzishwa kwa mfuko huu wa dharura mwaka 2005 ambao unapokea mchango wa hiyari kutoka nchi 129 pamoja na wadau wengine wa misaada, mamilioni ya watu wamepata msaada wa dola za Kimarekani bilioni 7 kwenye zaidi ya nchi 100 duniani, hii ikijumlisha zaidi ya dola bilioni 2.3 kwenye mizozo iliyopata ufadhili kidogo tofauti na uhitaji wake .