Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Cabo Delgado yaendelea kuwafungisha virago raia:IOM/UNHCR 

Mama akiwa amembeba mwanaye wakiwa wametawanywa na machafuko akienda kusaka maji kwenye kambi ya muda ya wakimbizi ya Montepuez Cabo Delgado Msumbiji
© UNHCR/Martim Gray Pereira
Mama akiwa amembeba mwanaye wakiwa wametawanywa na machafuko akienda kusaka maji kwenye kambi ya muda ya wakimbizi ya Montepuez Cabo Delgado Msumbiji

Machafuko Cabo Delgado yaendelea kuwafungisha virago raia:IOM/UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la uhamiaji duniani, IOM na la kuhudumia wakimbizi, UNHCR leo yameelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la machafuko katika jimbo la Cabo Delgado yanayopelekea watu kuendelea kukimbia makwao.

IOM inasema kati ya wakimbizi wa ndani 30,5000 kutoka Palma karibu robo tatu ni wanawake na watoto, mbako siku kadhaa mwezi uliopita  zaidi ya watu 1,000 waliwasili kila siku wakisafiri kwa basi, miguu, boti au ndege.  

Shirika hilo limeongeza kuwa fedha zinahitajika haraka kukabiliana na mahitaji ya dharura ya wakimbizi hao katika mgogoro ambao hadi sasa umeshafurusha na kutawanya watu wapatao 700,000 tangu kuzuka kwa mzozo Oktoba mwaka 2017. 

Mkurugenzi wa operesheni na masuala ya dharura wa IOM Jeff Labovitz amezuru Msumbiji wiki hii kutoa salamu zake za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika mashambulizi ya karibuni mjini Palma na kuonyesha mshikamano na raia waliotawanywa na jamii zilizoathirika na machafuko hayo  jimboni Cabo Delgado  

 Nayo UNHCR imesema mzozo katika jimbo hilo lililo na mafuta na gesi umesababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, kusambaratishwa kwa huduma na athari kwa raia hususan watoto ambao ni karibu nusu ya watu waliofurushwa.  

Limeongeza kuwa linatiwa hofu kubwa na athari za kibinadamu za mzozo huo na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia. 

“Tuna wasiwasi mkubwa wa athari za mzozo huu hasa kwa wanawake na watoto ambao ndio waathirika wa kubwa “ amesema mwakilishi wa UNHCR nchini Msumbiji. 

Shirika hilo linaendelea kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kibinadamu na serikali ya Msumbiji kuhakikisha kwamba maelfu ya wakimbizi wanapatiwa msaada muhimu unaohitajika ikiwemo malazi.