Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi milioni 1.9 wa Iraq katika maeneo yaliyoko katika hatari kubwa, kuchanjwa dhidi ya polio 

Mtoto aliyepokea chanjo dhidi ya polio awekwa alama kwenye kidole.
© UNICEF/Syed Mehdi Bokhari
Mtoto aliyepokea chanjo dhidi ya polio awekwa alama kwenye kidole.

Watoto zaidi milioni 1.9 wa Iraq katika maeneo yaliyoko katika hatari kubwa, kuchanjwa dhidi ya polio 

Afya

Mamlaka za afya za Iraq, kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa, la afya,WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF, jana jumapili wameanza kampeni kubwa ya kuwapatia chanjo watoto wa Iraq, ikiwalenga zaidi ya watoto milioni 1.9 chini ya umri wa miaka mitano.  

Taarifa ya WHO iliyotolewa hii leo Jumatatu katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, imesema kampeni hiyo itafanywa katika maeneo kote Iraq, licha ya janga linaloendelea la coronavirus">COVID-19 ambalo kama milipuko ya magonjwa ya hapo awali na dharura za kibinadamu limevuruga upatikanaji wa huduma muhimu za afya, pamoja na chanjo ya kawaida. Kampeni hiyo ni ya haraka na muhimu kwa sababu hata uingiliwaji mdogo wa programu za chanjo huacha watoto bila kinga, na kusababisha milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuiliwa na chanjo, kama vile polio na surua. 

Mwakilishi wa WHO nchini Iraq, Dkt Adham Ismail amesema, "ugumu wa kuhakikisha kuwa watoto nchini Iraq wanabaki salama kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiliwa na chanjo wakati huo huo kushughulikia COVID-19 ni mkubwa sana, lakini lazima tuendelee kufanya kila tuwezalo kulinda watoto dhidi ya mateso yanayoweza kuepukika na kifo kinachosababishwa  na ugonjwa unaoweza kuzuilika kwa chanjo. WHO na washirika wake wanafanya kazi kupita changamoto za COVID-19 kwa kuhakikisha mwendelezo wa juhudi za chanjo dhidi ya vitisho kwa watoto kama vile polio." 

Aidha Dkt Ismail amesema chanjo ya matone itafikishwa kote kwa njia ya mlango kwa mlango na katika vituo maalumu katika vituo vya afya ili kuhakikisha watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano wanafikiwa bila kujali hali yao ya awali ya chanjo na kwamba wanataka kuhakikisha hakuna mtoto ambaye ataachwa nyuma bila kujali kule waliko.   

WHO imesaidia mipango ya kuongoza timu za chanjo siku hadi siku, imehamasisha na kufundisha wasimamizi 862 na zaidi ya wachanjaji 4294 ili kutekeleza kampeni hiyo. Kwa kuongezea, pia WHO inalipa gharama zote za chanjo, pamoja na usafirishaji na motisha nyingine kuhakikisha kuwa watoto wote wanafikiwa. 

Kwa kuongezea, UNICEF imechangia shena yote ya chanjo ya polio kwa ajili ya kampeni hiyo na imetoa vifaa vinavyohitajika kuweka kipimo cha chanjo kwenye joto linalofaa, na hivyo kuhakikisha ufanisi wake. Aidha UNICEF imetengeneza pia vifaa vya elimu, kama vile video za habari na mabango, ili kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa chanjo na kuhamasisha walezi kuwachanja watoto wao. Kwa kuongezea, UNICEF imefundisha maafisa wa kujitolea 400 wa jamii kukuza uelewa, kufuatilia uvumi, na kupinga habari potofu kwa kutumia habari sahihi juu ya chanjo na faida zake. 

Kampeni hiyo ya siku 5 italenga watoto katika wilaya 46 katika majimbo16, pamoja na Baghdad (Baghdad-Resafa na Baghdad-Karkh), Babylon, Anbar, Dahuk, Erbil, Kerbala, Kirkuk Missan, Muthanna, Thi-Qar, Najaf, Ninewa, Salah Al-Din, Suleymaniya, Wassit na Basra. Maeneo hayo yalichaguliwa kulingana na hatari za kiafya kwa watoto katika kila moja, viashiria vya ufuatiliaji wa polio, hali ya chanjo ya watoto na mapungufu yaliyopo. Sababu zingine zinazozingatiwa ni pamoja na idadi ya watu, jiografia na hatari za mazingira.