Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Tigray, Ethiopia; Wakimbizi 4,000 wawasili kila siku Sudan

Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya nyumba yao kwenye eneo la Tigray nchini Ethiopia
© UNICEF/Tanya Bindra
Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya nyumba yao kwenye eneo la Tigray nchini Ethiopia

Mapigano Tigray, Ethiopia; Wakimbizi 4,000 wawasili kila siku Sudan

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesema mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa kabila la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo yanatia hofu kubwa kwa kuwa maelfu ya watu wanaendelea kukimbia na nusu yao wakiwa ni watoto. 

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema tangu kuanza kwa mapigano hayo mwanzoni mwa mwezi huu, zaidi ya watu 14,500 wakiwemo watoto, wanawake na wanaume wamekimbilia Sudan kusaka usalama na sasa kuna changamoto kubwa kuwapatia misaada ya kibinadamu. 

"UNHCR inatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo unaoendelea ziheshimu usalama na ulinzi wa raia huko Tigray," amesema Baloch.

Mapigano ya jana kwenye eneo hilo huko Ethiopia, yamekaribia eneo la kambi ya Shimelba ambayo inahifadhi takribani wakimbizi 6,500 kutoka Eritrea na hivyo kuibua hofu kuwa huenda wakimbizi wengi wakakimbia eneo hilo.

Kwa sasa UNHCR inaandaa kupokea wakimbizi ambao tayari wameanza kuingia kambi ya Hitsats iliyoko kilometa 50 kutoka kambi hiyo ya Shimelba na inapanga kuhamishia wengine kwenye maeneo mengine ya ukanda huo wa pembe ya Afrika.

Kwa mujibu wa Baloch, kwa ujumla mazingira ya UNHCR kuendesha operesheni zao ndani ya eneo la Tigray ni magumu kwa kuwa hakuna umeme na upatikanaji wa chakula na mafuta ni mgumu.

Hivi sasa mawasiliano yamekatwa na hivyo ni vigumu kupata taarifa.

Bwana Baloch amesema wakimbizi wanaosaka usalama Sudan wameongezeka haraka ambapo kwa siku zaidi ya wakimbizi 4,000 wanavuka mpaka kutoka Ethiopia na kuingia Sudan.

Wengi wao wanavuka kupitia mpaka wa Hamdayet ulioko jimboni Kassala na wengine wanapitia kituo cha mpakani cha Ludgi kilichopo jimboni Gedaref.

 Idadi ya wakimbizi wanaosaka usalama Sudan imeongezeka haraka ambapo kwa siku zaidi ya wakimbizi 4,000 wanavuka mpaka kutoka Ethiopia na kuingia Sudan- Babar Baloch, Msemaji UNHCR

Watu hao wanawasili wakiwa na virago vichache kwa kuwa wamefurushwa na mapigano huku watoto wakiwa wamechoka kupindukia.

UNHCR na wadau wake wanaimarisha usaidizi lakini idadi ya wanaowasili ni kubwa kuliko uwezo wa msaada unaotolewa.

Kituo cha mpito cha mapokezi eneo la Hamdayet kina uwezo wa kupatia malazi wakimbizi 300, ilhali tayari hivi sasa kimezidiwa uwezo kwa kuwa wakimbizi wamefika 6,000.

Hali ya mazingira ya usafi ni duni.

UNHCR imesema kwa wale wanaopitia mpakani Ludgi, wanapatiwa kwa muda malazi kwenye eneo liitwalo kijiij 8 kilichopo kilometa 35 kutoka mpakani mwa Sudan na Ethiopia.

Chama cha hilal nyekundu nchini Sudan kimetuma madaktari wake wakiwa na dawa muhimu kuelekea Hamdayet ili kufanya uchunguzi wa kiafya ikiwemo coronavirus">COVID-19 na mipango pia ya kuimarisha huduma za afya katika siku za usoni.

Kadri namba ya wakimbizi inavyoongezeka, serikali ya Sudan imeridhia kuanzishwa kwa kambi ya wakimbizi kwenye eneo la Um Rakuba, lililoko kilometa 80 kutoka mpakani, kambi ambayo itakuwa na uwezo wa kuhifadhi watu 20,000, huku maeneo mengine zaidi yakiandaliwa.