Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi ya Rwanda kuwapokea wakimbizi kutoka Libya-UNHCR

Picha ya maktaba, ni taswira kupitia dirisha la chuma ikionyesha mazingira ya wahamiaji waliolala kwenye magodoro sakafuni kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji nchini Libya
UNICEF/Romenz
Picha ya maktaba, ni taswira kupitia dirisha la chuma ikionyesha mazingira ya wahamiaji waliolala kwenye magodoro sakafuni kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji nchini Libya

Maandalizi ya Rwanda kuwapokea wakimbizi kutoka Libya-UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Maandalizi ya mwishomwisho yanaendelea kwenye kituo cha muda cha Gashora nchini Rwanda ambako kundi la kwanza la wakimbizi na waomba hifadhi lilitarajiwa kuwasiku juma hili. 

Pilikapilika za ujenzi zinaendelea kituoni Gashora ambapo kundi hilo lililotarajiwa kuwasili Septemba 26 mwaka huu ni la waomba hifadhi na wakimbizi wanaohamishwa kutoka kwenye vituo au mahabusu walikokuwa wakishikiliwa nchini Libya.

Serikali ya Rwanda , shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Muungano wa Afrika (AU) walitia saini muafaka mapema mwezi huu wa Septemba ili kuanzisha mkakati wa mpito kwa ajili ya kuwahamisha wakimbizi kutoka Libya.

UNHCR imesema chini ya muafaka huo serikali ya Rwanda itapokea na kutoa ulinzi kwa wakimbizi na waomba hifadhi ambao kwas asa wanashikiliwa katika vituo vya mahabusu nchini Libya.  

Kundi la kwanza la watu 75 wengi wakitokea Pembe ya Afrika, watahamishwa wakiwemo wanawake, Watoto na vijana walioko hatarini.

Baada ya kuwasili Rwanda UNHCR itaendelea kusaka suluhu zingine za kuokoa maisha kwa watu hao.

Na kisha watasafirishwa hadi Rwanda kwa mfumo wa hiyari. Akiwa kwenye kituo hicho cha Gashora Rwanda msemaji wa UNHCR Charley Yaxley amesema

(SAUTI YA CHARLEY YAXLEY)

“UNHCR inaitaka Jumuiya ya kimataifa kusaidia kituo hilki cha mpito hapa Rwanda lakini pia kuja na njia salama kama hizo ili tuweze kuwahamisha watu kutoka kwenye madhila nchini Libya.”

Shirika hilo limeshahamisha wakimbizi na waomba hifadhi 4,400 kutoka Libya na kuwapeleka katika nchi zingine tangu mwaka 217 wakiwemo 2,900 kupitia mkakati wa muda wa dharura nchini Niger na wengine 425 kwenda katika nchi za Ulaya kupitia kituo cha muda cha mapokezi nchini Romania.