Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde nchi za Ulaya ruhusuni wahamiaji waliomo kwenye meli wateremke- UNHCR

Mara nyingi wahamiaji husafiri kutoka Afrika kupitia bahari ya Mediteranea kwenda barani Ulaya
© UNHCR/Markel Redondo
Mara nyingi wahamiaji husafiri kutoka Afrika kupitia bahari ya Mediteranea kwenda barani Ulaya

Chonde chonde nchi za Ulaya ruhusuni wahamiaji waliomo kwenye meli wateremke- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limetoa wito kwa serikali za Ulaya ziwaruhusu wahamiaji na wakimbizi 507 wateremke kutoka katika meli iliyowaokoa kwenye eneo la kati la bahari ya Mediteranea.

Watu  hao waliookolewa hivi karibuni bado wamo kwenye meli hiyo ambapo UNHCR inasema wengi wao ni manusura wa vitendo vya kikatili nchini Libya na wamekimbia madhila nchini mwao.

Mwakilishi maalum wa UNHCR eneo la Mediteranea ya Kati Vincent Cochetel amesema, “watu hao wanahitaji msaada wa kibinadamu na baadhi yao tayari wameeleza nia yao ya kusaka hifadhi ya kimataifa.”

“Tunakimbizana na muda hivi sasa, mawimbi yanazidi kukumba eneo ambamo chombo chao kimetia nanga, na hali itazidi kuwa mbaya. Kuacha watu waliokimbia vita na ghasia nchini Libya kuendelea kusalia katika bahari kuu katika hali ya sasa ya hewa itakuwa ni kuongeza ‘chumvi kwenye kidonda,” amesema Bwana Cochetel.

Afisa huyo wa UNHCR amesema watu hao wanapaswa kuruhusiwa mara moja kuteremka kutoka kwenye meli hiyo na wapatiwe misaada ya haraka ya kibinadamu ambayo wanahitaji.

UNHCR inasema kuwa watu 151 bado wako kwenye meli hiyo Open Arms ilhali watu wengine 356 wamo kwenye meli nyingine iitwayo Ocean Viking.

Shirika hilo linasema kuwa nchi za Ulaya zitangaze ni bandari ipi ambapo meli hizo zinaweza kutia nanga na mataifa hayo yagawane jukumu la kuwahifadhi wahamiaji hao.

UNHCR imekumbusha jinsi ambavyo mwezi uliopita viongozi wa Ulaya walieleza kushtushwa kwao na tukio la kuuawa kwa watu zaidi ya 50 kwenye shambulio la anga kwenye kituo cha kushikilia mahabusu huko Tajoura nchini Libya ilhali watu wengine 150 wamekufa maji baharini Mediteranea.

“Hisia hizo sasa zinapaswa kutekelezwa kivitendo kwa kuonyesha mshikamano na watu wanaokimbia Libya,” amesema Bwana Cochetel akitaja hatua kama vile kuwapatia eneo la hifadhi na kanuni za kupata hifadhi kwa wale wanaosaka hifadhi ya kimataifa.

UNHCR inasisitiza kuwa mapigano makali yanayoendelea Libya sambamba na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo watu kushikiliwa kiholela ni ushahidi tosha kuwa eneo hilo si salama na hivyo mtu yeyote asiruhusiwe kurejea.