Vifo na uharibifu wa kimbunga Kenneth Comoro na Msumbiji vimenishtua:Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ripoti za vifo na uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Kenneth nchini Msumbiji na Comoro zimemshtua na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa fedha kukabiliana na mahitaji ya dharura na ya muda mrefu ya waathirika.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo Guterres amesema kimbunga Kenneth kimekuja wiki sita tu baada ya kimbunga kingine kikubwa Idai kilichosambaratisha maisha ya mamilioni ya watu Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA hadi sasa watu watato wametripotiwa kupoteza maisha nchini Msumbiji na watatu nchini Comoro.
Pia kimbunga hicho kimesababisha uharibifu mkubwa ikiwemo kuharibi asilimia 90 ya nyumba kwenye jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, kuezua mapaa ya nyumba, kubomoa madaraja na kuharibu miundombonu mingine ikiwemo nguzo za umeme Comoro na Msumbiji. Na mafuriko zaidi yanatarajiwa Msumbiji.
Katibu Mkuu Guterres ametuma salamu za rambirambi na mshikamano kwa familia za walioathirika, serikali na watu wa Msumbiji na Comoro.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wanazisaidia mamlaka katika kutathmini mahitaji na kutoa msaada.
Katibu Mkuu ametoa ombi kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza rasilimali fedha ambazo zinahitajika haraka ili kushughulikia mahitaji ya dharura, ya muda mfupi na ya muda mrefu.
Katibu Mkuu anatarajiwa kuzuru hivi karibuni nchini Msumbiji kufuatia ombi maalum la Rais Filippe Nyusi wa nchi hiyo.