Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lori la chakula cha msaada lashambuliwa Hodeidah:WFP

Watu maelf kadhaa wakiwa wanahitaji msaada, msururu wa magari kama huu wenye shehena  ya msaada wa lishe upo ingawa mara kwa mara huwa inashambuliwa.
WFP/Marwa Awad
Watu maelf kadhaa wakiwa wanahitaji msaada, msururu wa magari kama huu wenye shehena ya msaada wa lishe upo ingawa mara kwa mara huwa inashambuliwa.

Lori la chakula cha msaada lashambuliwa Hodeidah:WFP

Amani na Usalama

Shirika  la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani,  WFP limesikitishwa na shambulio dhidi ya lori lililolkuwa limebeba chakula cha msaada  likitokea mjini Hodeidah kuelekea wilaya ya Al Tuhayta kusini mwa Yemen.

Shirika hilo limesema wakati lori hilo linashambuliwa lilikuwa na nembo ya WFP iliyokuwa inaoenakana wazi na lilikuwa limesheheni tani 30 za chakula cha msaada, ambacho kingetosheleza kuwalisha watu 2,000 kwa muda wa mwezi mzima. Shambulio hilo limefanywa na kundi lisilojulikana lililojihami kwa silaha umbali wa kilomita mbili tu  kutoka mahali  lilipokuwa linakwenda.

Dereva wa lori hilo alijeruhiwa na kukimbizwa hospitail ya Al Khawkha na hali yake hivisasa, inasemekana  kuendelea vizuri wakati lori lilisalia palepale na shehena kuhamishiwa kwenye gari linguine ambapo hatimaye kufika palipotarajiwa.

Shirika la WFP limetoa wito kwa pande zote kinzani kuwalinda raia wa kawaida, kuheshimu misingi ya kibinadamu na pia kuruhusu chakula cha  msaada kipite kwa amani ili kiwafikie walengwa, bila kujali wako wapi hususan katika maeneo yaliyo na mapigano.

Makabiliano makali katika wilaya za Al Tuhayata na Al Duraihimi yamezuia msaada wa chakula  kuwafikia watu ambao wamenaswa  katika eneo hilo tangu mwezi Juni ambao WFP inaamini wako katika hali  taabani.

 Hata hivyo siku chache zilizopita WFP  ilifanikiwa kufikisha chakula kwa watu 33,000sawa na karibu nusu ya watu wa Al Tuhayta.

Yemen ndio nchi iliyo na zahma kubwa ya njaa duniani ambapo watu theluthi mbili au watu milioni 18 hawajui watapata wapi mlo unaofuata.