Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na WMO kudhibiti athari za kiafya na hali ya hewa

Picha ya shirika la afya ulimwenguni ikionyesha mtu mwenye magonjwa ya njia ya hewa

WHO na WMO kudhibiti athari za kiafya na hali ya hewa

Afya

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamekubaliana kuanzisha  mkakati maalum wa pamoja utakaosaidia kudhibiti athari za kiafya zinazosababishwa na mazingira duni.

Mashirika hayo, lile la afya WHO na lile la hali ya hewa, WMO yamesema mazingira duni yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi husababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 12.6 kila mwaka.

Makubaliano hayo mapya yaliyoridhiwa mjini Geneva, Uswisi kati ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus na Katibu Mkuu wa WMO Dkt. Petteri Taalas, yatajikita katika kukuza uelewa kwa undani, jinsi ya kutatua changamoto hizo za kiafya zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi ya  muda mrefu.

Mathalani yatatoa kipaumbele katika ufuatiliaji wa hatari za afya zitokanazo na mazingira, kama vile mionzi mikali ya jua aina ya UV, hewa chafu pamoja na maji yasiyo safi na salama.

Dkt. Taalas amesema utafiti umebaini kuwa kimbunga Maria kilichopiga Puerto Rico na kusababisha vifo vya watu 64 kinahusishwa pia na vifo vingine vya watu 4,645 vilivyosababishwa na ukosefu wa huduma za afya, kukatika kwa umeme na uharibifu wa miundombinu mingine.

Naye Dkt. Tedros amesema kila mwaka zaidi ya watu milioni 12 hupoteza maisha kutokana na kutumia maji machafu, kuvuta hewa chafu na kemikali mbalimbali hewani.

TAGS: WMO, WHO, mazingira, afya