Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio dhidi ya Marekani lapita, yenyewe yasema halina maana

Matokeo ya kura ya azimio la Baraza Kuu la kuitaka Marekani ibadili uamuzi wake wa kutambua Yerusalem kama mji mkuu wa Israel. 128 wamekubali, nchi 9 zimepinga huku nchi 35 hazikuonyesha msimamo wowote. Nchi nyingine 21 hazikutokea barazani. (Picha:UN /Manuel Elias)

Azimio dhidi ya Marekani lapita, yenyewe yasema halina maana

Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Alhamisi uligubikwa na maneno ya vijembe wakati wawakilishi wa nchi 193 wanachama wa Umoja huo walipokuwa wanatoa maoni yao kabla ya kupiga kura ya kutaka Marekani ibadili uamuzi wake wa kutambua Yerusalem kama mji mkuu wa Israel. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora Nducha)

Je Yerusalem utakuwa au ni mji mkuu wa Israel?

Ni sakata lililotawala baraza kuu la umoja wa Mataifa hii leo katuika kikao cha dharura mjini New york Marekani.

Kila mwamba ngozi akivutia kwake..

image
Balozi Danny Danon, mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Manuel Elias)
Balozi Danny Danon, mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Balozi Danon)

Hakuna azimio la UNESCO, hakuna hotuba zisizo na chochote , hakuna kura ya baraza kuu itakayotutenganisha na Yerusalemu.”

image
Balozi Nikki Haley, Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.(Picha:UN/Manuel Elias)
Marekani iliyozua songombingo yote hii imeapa asilani abadani wembe ni uleule.

(Sauti ya Balozi Nikki Haley)

Ubalozi wetu utahamia Yerusalemu, hakuna kura yoyote kwenye Umoja wa Mataifa itakayobadili hilo.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad Al Malik akafunguka..

image
Riad Al-Malki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Manuel Elias)
(Sauti ya Riyad Al Malik)

Uamuzi huu hautoathiri hali ya Yerusalemu lakini utaathiri nafasi ya Marekani kama msuluhishi wa amani.

Na baada ya nchi wanachama kueleza misimamo yao, kura ikapitwa, na rais wa Baraza Kuu Miroslav Lacjack akatangaza matokeo..

(Nats..)

Anasema kuwa wanachama 128 wameunga mkono azimio la kutaka Marekani ibadili uamuzi wake wa kutambua Yerusalem kama mji mkuu wa Israel, huku nchi 9 zimepinga, ilhali nchi 35 hazikuonyesha msimamo wowote.

image
Matokeo ya kura ya azimio la Baraza Kuu la kuitaka Marekani ibadili uamuzi wake wa kutambua Yerusalem kama mji mkuu wa Israel. 128 wamekubali, nchi 9 zimepinga huku nchi 35 hazikuonyesha msimamo wowote. Nchi nyingine 21. (Picha:UNwebvideo capture)
Nchi zilizounga mkono ni pamoja na Tanzania, Burundi na Botswana ilhali Rwanda na Uganda hazikuonyesha msimamo wowote.

Katika upigaji kura huo nchi 21 hazikutokea katika ukumbi wa Baraza Kuu ikiwemo Kenya, Zambia, Swaziland na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine linasisitiza kuwa uamuzi wowote au vitendo vinavyolenga kubadili hadhi na mjumuiko wa mji mtakatifu wa Yerusalem hauna mashiko yoyote kisheria na ni batili.

Na zaidi ya yote hatua yoyote kwa mji huo ni lazima izingatie maazimio ya awali  ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo basi nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ni lazima zijiepusha na kujenga balozi zao kwenye mji mtakatifu wa Yerusalem.

Na je hatua hii ya leo ina maana gani? Flora Nducha amezungumza na Dkt. Salim Ahmed Salim, mwanadiplomasia nguli kutoka Tanzania ambaye pia amewahi kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1979.