Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzorota kwa usalama CAR kwatishia usalama wa watoto: UNICEF

Ustawi wa watoto kama hawa wa CAR uko mashakani kwa sasa. (Picha:UN/Cristina Silveiro)

Kuzorota kwa usalama CAR kwatishia usalama wa watoto: UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema kuanza upya kwa mapigano huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kunatishia ustawi wa watoto nchini humo.

UNICEF imetaja maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo ambako hakuna utulivu pamoja na mji mkuu Bangui ambako ghasia zimehusisha pia mashambulizi dhidi ya watoa huduma za kibinadamu.

Shirika hilo limesema matukio yalishika kasi zaidi kati ya tarehe Saba na 19 mwezi wa Oktoba ambapo kulikuwepo na matukio Saba na hivyo kukwamisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Zaidi ya watoto Milioni2.3 wameathiriwa na mzozo wa CAR tangu mapigano makali yabishe hodi Bangui mwezi Disemba mwaka.

Christophe Boulierac ni msemaji wa UNICEF, Geneva.

(Sauti ya Boulierac)

“Watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji msaada na wako hatarini kusahaulika. Tuanhitaji uwezo wa kusafirisha misaada kwa usalama na bila kikwazo chochote ili tuwafikie watoto hao walio hatarini zaidi na familia zao. Na tunatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kutuhakikishia uwezo wa kuwafikia watu hao wenye uhitaji.”

Wakati huo huo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema kwa sasa upelekaji wa misaada kwa wahitaji hususan maeneo ya vijijini ni changamoto kubwa.

Shirika hilo limesema kiwango cha akiba ya chakula huko vijijini kiko chini ya asilimia 50.