Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azidi kulaani kuongezeka kwa mapigano Syria

Ban azidi kulaani kuongezeka kwa mapigano Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea kusononeshwa kwake na mapigano yanayozidi kuongezeka nchini Syria hususani Aleppo ambapo ripoti zinasema raia ni miongoni mwa mamia ya watu waliouwawa na kujeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa ofisi ya Katibu Mkuu alhamisi mjini New York, inaeleza kuwa Katibu Mkuu Ban amelaani kile alichokiita kuongezeka kiholela kwa matumizi ya silaha nzito na makombora katika sehemu za raia. Bwana Ban amesisitiza kulaani matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini kutoka kwa vikosi vya serikali hivi karibuni mjini Allepo.

Bwana Ban amesema wakati juhudi za kuzileta mezani pande zote zinzopingana nchini Syria zikiendelea , kuendelea kwa machafuko kutanufaisha wale tu wanaoamini kwamba njia za kijeshi ndio muafaka wa mgogoro huo kwa kugarimu maisha ya watu wa Syria ambao tayari wameshateseka. Ametaka pande zote kuwaachilia wale walioko vizuizini na kukomeshwa kuzingira raia pamoja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wenye mahitaji.

Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema jambo muhimu ni pande hizo kupunguza machafuko na kujielekeza katika kufikia amani kwa suluhu ya kisiasa.