Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Wapatanishi wa UM/UA kwa Darfur waripoti mbele ya BU juu ya hali ya amani kieneo

Wapatanishi wa UM na UA juu ya Darfur, yaani Jan Eliasson na Salim Ahmed Salim wamewasilisha ripoti zao mbele ya Baraza la Usalama kuhusu hali ya usalama na amani kwenye jimbo hili la mgogoro la Sudan magharibi. Mpatanishi wa UM Eliasson alisema kwenye risala yake kwamba yeye na Mpatanishi wa AU Salim wamependekeza kwa KM ateuliwe Mjumbe Maalumu juu ya Darfur, atakayekuwa na makao yake Khartoum, Sudan kushughulikia suala hilo, na wao wapo tayari kumsaidia mwakilishi huyo kwa kila njia kuleta amani kwenye jimbo la mgogoro.

Mwendesha Mashtaka wa ICC anasihi Lubanga asiachiwe

Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) ametoa mwito maakumu unaowanasihi majaji wa korti hiyo kutomwachia mtuhumiwa wa kwanza wa mahakama, Thomas Lubanga aliyekuwa kiongozi wa majeshi ya mgambo katika JKK (DRC). Majaji wa Mahakama ya ICC wanazingatia kumwachia Lubanga kwa sababu ushahidi uliowakilishwa kwenye kesi yake ulikuwa na kasoro kisheria, dhidi yake. Miongoni mwa mashtaka aliotuhumiwa Lubanga ni lile kosa la kuwashirikisha watoto chini ya umri wa miaka 15 kwenye shughuli za vita na mapigano, katika eneo la mamshariki la Ituri, katika JKK. Mtuhumiwa amekataa makosa.~

Hapa na Pale

Baraza la Usalama limekutana kusailia na kushauriana juu ya operesheni za Shirika la UM linalosimamia usitishwaji wa mapigano mipakani Ethiopia na Eritrea (UNMEE), na pia kuzingatia hatua za kuchukuliwa siku za mbele na jamii ya kimataifa kuhusu ulinzi wa eneo hilo.

Hali ya kisiasa Zimbabwe yapewa usikizi mkubwa na BU na KM

Alasiri Baraza la Usalama lilikutana, kwenye kikao cha hadhara/faragha, kujadilia hali halisi ya kisiasa nchini Zimbabwe kufuatia uamuzi wa Morgan Tsvangirai, wa chama cha upinzani cha MDC, kujitoa kugombania uchaguzi wa urais ambao unatarajiwa kufanyika nchini mwisho wa wiki. KM wa UM, Ban Ki-moon, katika risala yake kuhusu suala hili, alioitoa kwa kupitia Msemaji wake, alisema anakhofia kitendo cha kiongozi wa MDC kujitoa kwenye uchaguzi kinatia "wasiwasi wa kina" na hakiashirii mema kwa mfumo wa demokrasia katika Zimbabwe.

Darfur inakabiliwa na janga la kiutu "timilifu", mashirika ya UM yaonya

Mashirika ya UM yaliopo kwenye eneo la Sudan magharibi la Darfur limetahadharisha kwenye taarifa iliotolewa ya pamoja kwamba hali iliojiri Darfur sasa hivi inaelekea kuzusha "dhoruba timilifu" ya matatizo ya kiutu, hususan yale matatizo yanayoambatana na upungufu wa chakula, halia ambayo imekorogwa zaidi kwa sababu ya kuongezeka kwa fujo na vurugu kieneo, na pia kufurika kwa kambi za umma uliong\'olewa makwao, ikichanganyika na mavuno haba katika mwaka huu.

Mfanyakazi wa UNHCR Usomali ametekwa nyara

Mfanyakazi mzalendo wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) nchini Usomali, Hassan Mohamed Ali, alitekwa nyara Ijumapili usiku kutoka nyumbani kwake, katika vitongoji vya mji mkuu wa Mogadishu na kundi la watu wenye silaha wasiotambulikana ambao walimchukua kwenye eneo lisiojulikana. Kwenye taarifa iliotolewa juu ya tukio hilo, UNHCR ilisema sababu za kutoroshwa kwa mfanyakzi wao huyo nazo pia hazijulikani.

Zawadi ya UM juu ya Huduma za Jamii kutunzwa taasisi 12 za kimataifa

Tarehe 23 Juni huadhimishwa kila mwaka na UM kuwa Siku ya Kuheshimu Mchango wa Huduma za Umma Kimataifa. Jamii ya kimataifa, kwa kuiadhimisha siku hiyo, ilizitunukia taasisi 12 za kimataifa Zawadi ya 2008 ya UM Kuhusu Huduma za Umma, taasisi ambazo kwa mchango wao kwenye huduma za kijamii zilifanikiwa kufaidisha maisha mema kwa watu wa kawaida wanaoishi kwenye maeneo yao.

Mukhtasari wa Mkutano wa Norway kwa Wanaharakati Vijana Kutunza Mazingira

Mkutano wa Watoto wa Kimataifa wa Tunza unaofanyika kwenye mji wa Stavanger, Norway kuanzia tarehe 17 hadi 21 Juni uliandaliwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) pamoja na Shirika lisio la Kiserekali la Norway linaloitwa Ajenda ya [Karne ya] 21 kwa Vijana, wakichanganyika na wafadhili wengine wa kimataifa. Mkutano ulikusanyisha vijana 700 wa umri kati ya miaka 10 mpaka 14, wakiwakilisha zaidi ya nchi 100, ambao waliongozwa na watu wazima 300.

Siku ya Wahamiaji Duniani Inaadhimishwa Kimataifa

Tarehe 20 huadhimishwa kila mwaka kimataifa, kuwa ni Siku ya Wahamiaji Duniani – siku ambayo umma wa kimataifa huheshimu na kukumbushana juu ya jukumu liliodhaminiwa Mataifa Wanachama na Mkataba wa UM kuhudumia kihali na mali umma wenziwao uliong\'olewa kwa nguvu makwao kwa sababu wasioweza kuzidhibiti. Kadhalika mnamo siku hiyo walimwenngu huheshimu mchango wa wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa wanaoshughulikia ugawaji wa misaada ya kiutu kwa wahamiaji hawo.