Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

KM anajiandaa kuzuru Asia

KM Ban Ki-moon anatarajiwa kuanza ziara ya siku 12 katika bara la Asia kuanzia kesho Ijumaa ambapo pia atahudhuria Mkutano Mkuu wa Mataifa Wanachama wa Kundi la G8 utakaofanyika Ujapani.

Nowak ainasihi Zimbabwe kusitisha mateso na fujo

Manfred Nowak, Mkariri Maalumu wa UM juu ya Masuala ya Mateso na Vitendo Katili vya Kuadhibu na Kudhalilisha Utu ametoa mwito kwa Serikali ya Zimbabwe na jumuiya ya kimataifa wajumuike kipamoja, kidharura, kufanya kila wawezalo kusitisha haraka fujo na vitendo vya mateso nchini humo dhidi ya raia.

Hapa na pale

Baraza la Usalama, kwenye taarifa ya raisi kwa mwezi Juni, limeyasihi makundi yote yanayohasimiana Sudan Kusini kutumia mwongozo wa \'ramani ya mapatano\' yaliofikiwa Juni 8 kwenye yale Maafikiano ya Jumla ya Amani, ili kuzima cheche za fukuto liliozusha fujo za karibuni kwenye mji wa Abyei.

UM inasema wanawake wanahitajia kinga imara dhidi ya mateso

Taasisi za UM zinazoshughulikia juhudi za kimataifa za kukomesha mateso na kusaidia waathiriwa wa janga hili, zimetoa taarifa muhimu yenye kusisitiza kwamba walimwengu bado watahitajia kuchangisha bidii zao kwa wingi zaidi ili kufanikiwa "kuwapatia kinga na hifadhi madhubuti kila mwanadamu mstahiki dhidi ya mateso" licha ya kuwepo ulimwenguni kwa vyombo kadha wa kadha vya sheria ya kimataifa vinavyoharamisha janga hilo.

Mkuu wa Idara ya Usalama ya UM Kajiuzulu

David Veness, KM Mdogo anayehusika na Masuala ya Ulinzi na Usalama wa UM amemuarifu KM kwamba ameamua kujiuzulu, kwa khiyari, kwa sababu anaamini ilivyokuwa yeye ndio mwenye dhamana ya shughuli za Idara ya Usalama, ambayo ilishindwa kudhibiti hifadhi bora ya majengo ya UM mjini Algiers na kuashiria uwezekano wa kushambuliwa, aliwajibika kuwacha madaraka baada ya shambulio maututi la kigaidi kwenye majengo ya UM Algiers mnamo Disemba 2007.

UNHCR inashinikiza mfanyakazi aliotekwa nyara Usomali aachiwe

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuwa linaendelea kushinikiza, kwa sauti kuu, aachiwe huru yule mfanyakazi wao, Hassan Mohammed Ali, ambaye alitekwa nyara Ijumamosi iliopita kutoka nyumbani kwake katika mji wa Afgooye, kilomita 30 kutoka Mogadishu, na watu wasiojulikana. Kwa mujibu wa UNHCR mateka Ali aliweza kuzungumza kwa simu na aila yake Ijumapili usiku na alisema hali yake ni nzuri; lakini taarifa nyengine ziada yoyote kuhusu mahali alipo na utambulisho wa makundi yaliomtorosha haijulikani. ~

BU kushtumu fujo na utumiaji mabavu Zimbabwe

Ijumatatu usiku, Baraza la Usalama liliafikiana, kwa kauli moja, kushtumu kampeni ya utumiaji mabavu inayoendelezwa na wenye madaraka Zimbabwe, dhidi ya wapinzani wa kisiasa, na pia kulaani vitendo vya Serikali ambavyo inaripotiwa huwanyima wapinzani haki ya kuendeleza kampeni huru za uchaguzi. Kwenye taarifa iliotolewa baada ya majadiliano ya faragha katika Baraza la Usalama, Raisi wa mwezi Juni wa Baraza, Balozi Zalmay Khalilzad wa Marekani alisema wajumbe wa Baraza wanaamini fujo iliotanda sasa hivi Zimbabwe, ikichanganyika na vikwazo dhidi ya vyama vya upinzani, ni hali ambayo uchaguzi ulio huru na wa haki hauwezekani kufanyika abadan, uchaguzi ambao umetayarishwa ufanyike Juni 27 (2008).