Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Kenya: UNICEF yapatia wakazi wa Kaunti ya Mto Tana fedha za kujikimu

Mafuriko Kenya: UNICEF yapatia wakazi wa Kaunti ya Mto Tana fedha za kujikimu

Pakua

Mvua za El-nino zikiendelea kutikisa ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo taifa la Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo kwa ufadhili wa serikali ya Uingereza limepatia msaada wa hali na mali wakazi wa kaunti ya mto Tana walioathiriwa na mafuriko hayo.  Cecily Kariuki na taarifa zaidi.

Video ya UNICEF Kenya inaanza ikimuonesha mkazi huyu wa hapa mji wa Garseni katika kaunti ya mto Tana akiwa amebeba kikapu huku akiwa na watoto wake wawili wakirejea nyumbani.

Huyu si mwingine bali Eva Ghahamaro akisimulia yaliyowasibu na msaada ulivyowafikia. Anasema, “Maisha yalikuwa magumu kwa sababu mafuriko yaliharibu nyumba na mashamba. Vyakula vilisombwa. Watu wengi waliteseka sana. Maafisa wa kaunti waliona tunateseka, walitembea nyumba kwa nyumba wakisajili majina watu wenye watoto na wajauzito. Nilikuwa nikipata shilingi 2,750.”

Shilingi 2750 ni sawa na dola 20 za kimarekani, na wanapatiwa kila mwezi. Rachael Wamoto ni afisa kutoka UNICEF Kenya na anafafanua kuhusu usaidizi huo ambao haukulenga tu waathiriwa wa mafuriko bali pia kaya zenye watoto walio na utapiamlo.

“Kwa programu hii tuko katika kaunti sita. Kwa kaunti ya Mto Tana tumeweza kufikia kaya 1,800 (Elfu Moja Mia Nane) katika miji ya Galole na Garsen. Vikundi kazi vya Kaunti ndio vilihusika kwenye kuchagua kaya zenye uhitaji. Hivyo tuliweza kutambua watu walioathiriwa na mafuriko na waliokimbia makwao. Tunashirikiana na serikali na mamlaka ya taifa ya udhibiti wa ukame. Tuliweza kutumia orodha yao na hivyo kufikia haraka wahitaji.”

Msaada wa fedha taslimu uliofadhiliwa na serikali ya Uingereza, umekuwa na manufaa kwa Eva. Akisema twins, anamaanisha watoto mapacha.

“Nilitumia hizo fedha kununulia wanangu chakula, uji, mkaa na pia mahindi na mchele kwa familia yangu. Halikadhalika, watoto wangu hawa mapacha niliwaandikisha shule nikawanunulia sare na mabegi ya shule. Nimeshukuru sana UNICEF kwa msaada wao kwa sababu mmetusaidia.

Audio Credit
Cecily Kariuku
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
UNICEF/Jame Ekwam