Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Watoto walioko Rafah wasihamishwe kwani tayari wako taabani

UNICEF: Watoto walioko Rafah wasihamishwe kwani tayari wako taabani

Pakua

Janga la kibinadamu likizidi kushamiri kila uchao huko Ukanda wa Gaza, shirika la  Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaonya kuwa kuzingirwa kijeshi kwa eneo hilo sambamba na operesheni za ardhini za kijeshi huko Rafah kutasababisha janga kubwa kwa watoto 600,000 waliosaka hifadhi kwenye eneo hilo. 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini New York, Marekani inakumbusha kuwa amri ya kuhamia Rafah, kusini mwa Gaza iliyotolewa mwezi Oktoba mwaka jana na Israel imefanya eneo hilo sasa kuhifadhi watu wapatao milioi 1.2, nusu yao wakiwa ni watoto wakiishi kwenye mahema au nyumba zisizo kamilifu.

Kwa kuzingatia mlundikano wa watoto, wakiwemo wengi walio hatarini wakihaha kuishi, pamoja na ukubwa wa ghasia zinazoendelea na njia za kutumia kukimbia zikiwa na vilipuzi au hakuna njia kabisa , UNICEF inaonya madhila zaidi kwa watoto na operesheni za kijeshi vitaongeza vifo zaidi vya raia na miundombinu ya huduma za msingi iliyosalia kusambaratishwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema zaidi ya siku 200 za vita zimekuwa ‘mwiba’ kwa watoto na Rafah hivi sasa ni mji wa watoto wasio na pahala salama pa kukimbilia Gaza. Iwapo operesheni kubwa za kijeshi zikianza, watoto sio tu watakuwa hatarini na ghasia, bali pia vurugu na kiwewe wakati ambapo hali zao kimwili na kiakili zimeshadhoofishwa.

Hivyo UNICEF inasisitiza wito wa Kamati ya Mashirika ya UN kwa Israel ya kuzingatia wajibu wake kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu ya kupatia chakula na matibabu watoto na kuwezesha operesheni za kugawa misaada na kwa viongozi wa dunia kuzuia janga zaidi kwa watoto Gaza sambamba na sitisho la mapigano.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'39"
Photo Credit
© UNOCHA/Ismael Abu Dayyah