Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa umeanza kufikisha misaada kwa wakimbizi ili kujiandaa na mafuriko

Umoja wa Mataifa umeanza kufikisha misaada kwa wakimbizi ili kujiandaa na mafuriko

Pakua

Tukiwa katika msimu wa mvua kwa nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara, tuelekee nchini Somalia, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA limesema wao na wadau wao wamejiandaa kufikisha mahitaji kwa watu 770,000 katika wilaya 22 za nchi hiyo ambao wanatarajiwa kuathirika na mvua za msimu huku wakieleza kuwa wakimbizi wa ndani wanatarajiwa kuaahirika ziadi.

Katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Matal Amin iliyoko Baidoa nchini Somalia zaidi ya wananchi 1500 wanahaha huku na kule kurekebisha maturubai yao ambayo hasa ndio makazi yao ikiwa ni maandalizi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kuanza muda wowote. 

Hali ni hivyo hivyo pia katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Rama cade kama anavyotueleza Kiongozi wa kambi hiyo Abdulkadir Adinur Aden anasema “Tunajiandaa na msimu wa mvua ili kupunguza athari za mafuriko, tunatumia maturubai ya plastiki kufunika makazi yetu na pia tunatumia viroba vilivyojazwa michanga ili kuzuia mnomonyoko mafuriko yatakapo tukumba.”

Wadau mbalimbali wa misaada ya kibinadamu ikiwemo OCHA wamepeleka katika kambi hizo misaada kama vile chakula na lishe, viroba vilivyojazwa michanga, maji safi na salama pamoja na dawa mbalimbali ikiwemo za kipindupindu hata hivyo mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa OCHA nchini Somalia Erich Ogoso anasema mengi ya makazi hayataweza kuhimili mvua kubwa na hivyo yataharibiwa.

“Wananchi wanaoishi katika kambi hii ya Matal Amin walifika hapa mwaka 2017 wakitokea katika mkoa wa Bay ambako walikimbia ukame, mzozo, na mambo mengine. Wamekuwa wakiishi hapa tangu kipindi hicho, mafuriko yanapokuja wamekuwa wakiondoka eneo hili na kukikauka wanarejea na sasa wanajiandaa tena na mafuriko na kuna uwezekano wakutakiwa kuondoka eneo hili.” 

OCHA wanasema taarifa walizopokea kutoka kwa wadau wao walioko mashinani mpaka kufikia tarehe 28 mwezi Aprili mwaka huu, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Somalia zimewaathiri zaidi ya watu 124,155 na kuwaacha zaidi ya 5,130 bila makazi huku vifo vya watoto saba vikiripotiwa. 

Audio Credit
Leah Mushi
Sauti
2'17"
Photo Credit
© UNOCHA/Ayub Ahmed