Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtu 1 kati ya 5 katika nchi 59 duniani anahitaji hatua za haraka kuepushwa na baa la njaa: FAO

Mtu 1 kati ya 5 katika nchi 59 duniani anahitaji hatua za haraka kuepushwa na baa la njaa: FAO

Pakua

Ripoti mpya ya kimataifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO kuhusu mgogoro wa chakula duniani inasema karibu watu milioni 282 walio katika nchi 59 walikabiliwa na viwango vya juu vya njaa mwaka 2023. 

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Asante Leah. Kwa hakika ripoti hiyo ya “Mgogoro wa kimataifa wa chakula” GRFC inasema kiwango cha watu wenye njaa duniani kiliongezeka kwa watu milioni 24 kutoka mwaka 2022 hadi 2023 na ni asilimia 21.5 ya watu waliofanyiwa tahimini  na hicho ni kiwango kikubwa sana ukilinganisha na ilivyokuwa kabla ya janga la COVID-19 limesema shirika la FAO likiongeza kuwa idadi ya walio na njaa duniani inaendelea kuongezeka.

Ripoti imetaja sababu kuu tatu ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa janga la njaa duniani ambazo ni mosi migogoro na vita ambapo inasema inaathiri katika nchi 20 zilizo na jumla ya watu milioni 135 wanaokabiliwa na njaa zikiwemo Sudan, Yemen na Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Pili ni matukio mabaya ya hali ya hewa yaliyochangiwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa chanzo cha njaa katika nchi 18 na kuathiri kwa njaa zaidi ya watu milioni 77.

Na tatu mdororo wa kiuchumi uliokuwa chachu ya njaa katika nchi 21 na kuathiri jumlaya watu milioni 75.

FAO imesema kwa miaka minne mfululizo takriban asilimia 22 ya watu waliofanyiwa tathimini duniani wamekuwa wakikabiliwa na kutakuwa na uhakika wa chakula. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Mgogoro huu unahitaji hatua za haraka. Kutumia takwimu zilizoainishwa katika ripoti hii ili kufanyia marekebisho mifumo ya chakula na kushughulikia mizizi ya kutakuwa na uhakika wa chakula itakuwa muhimu sana”

Kwa mujibu wa ripoti waathirika wakubwa ni watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mtandao wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa chakula imetoa wito wa haraka wa kubadili mtazamo ili ujumuishe amani, hatua za kuzuia na za maendeleo sambaba na juhudi za dharura kuvunja mzunguko wa janga la njaa ambalo linasalia katika viwango vya juu

 

Audio Credit
Leah Mushi / Flora Nducha
Sauti
2'23"
Photo Credit
Nearly 18 million people across Sudan are facing acute hunger.