Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Niger ILO yanusuru wanawake na mfumo wa utumwa

Nchini Niger ILO yanusuru wanawake na mfumo wa utumwa

Nchini Niger mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani la kujengea uwezo jamii zinazotumikishwa umeweza kunusuru maisha ya jamii hizo ambazo awali zilionekana hazina thamani kwenye jamii, lakini sasa sio tu zina uwezo wa kiuchumi bali pia zinatambua haki zao na kujua kusoma na kufanya mahesabu. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Kutana na Hadjara Hamidou, mkazi wa kijiji cha Mazague jimboni Agedez nchini Niger, anasema kabla ya ujio wenu tuliishi kwenye machungu. Kulikoni?

Hadjara ni waathiriwa wa mfumo wa utumwa uitwao Wahaya unaotekelezwa hadi sasa nchini Niger. Anasema chini ya mfumo huo wazee na wazazi wake walikuwa watwana na walionekana kama mbwa. Mfumo huo wa utumwa wa Wahaya unahusisha mwanamke aliyetokea kwenye familia ya watumwa, kununuliwa na mwanaume mwenye wake wengi na mtumwa huyo anatumikishwa kwenye familia hiyo.

Hadjara anasema mimi sikuolewa na nimekuwa naishi peke yangu kwa miaka mingi na kwamba mtaani akipita anatukanwa kuwe yeye ni mtumwa mchafu. Lakini ujio wa mradi wa ILO umebadilisha yote hayo. 

Mradi huo wa ILO pamoja na kuwaelimisha kuhusu haki zao za msingi, uliwapatia mafunzo ya ujasiriamali, ikiwemo ufugaji wa mifugo kama vile mbuzi na kuku na pia kuongeza thamani ya mazao kama vile maziwa ya mbuzi. Na zaidi ya yote..

Anasema ninafahamu kuhusu haki zangu na ninahakikisha zinaheshimiwa. Nafahamu kwa mfano jinsi ya kufungua mashtaka iwapo ninatukanwa. Asanteni kwa kila kitu, anasema Hadjara, akiongeza kuwa asante sana kwani ujio wenu umemaliza manyanyaso. Leo hii hatuzungumzii tena mambo hayo hapa kijijini.”

Hii leo Hadjara hii kijiini kwao anaonekana kuwa mwanamke jasiri na ambaye hajakosa kitu chochote. 

Pamoja na ujasiriamali, Hadjara amejifunza pia kusoma na kuandika lugha ya kifaransa na pia kufanya mahesabu. Amejifunza pia kutengeneza jibini kutokana na maziwa ya mbuzi. 

Ndoto yangu ni siku moja mradi huo uwe mkubwa na aweze kufungua duka kubwa la kuwezesha wanakijiji kupata bidhaa zote hapo, na yote ni kwa sababu ya mradi wa ILO.

Hadjara anamalizia kwa kutoa shukrani kwa wote waliowezesha kufanikisha kwa mbinu hiyo na kwamba Mungu awabariki.

Mradi huo umefikia zaidi ya wanawake 400 waliokuwa wanaathiriwa vibaya na mfumo wa utumwa wa Wahaya kwenye majimbo ya Tahoua na Agadez nchini Niger.

Kwa mujibu wa ILO, ufadhili wa mradi huu umewezeshwa na serikali ya Marekani.

 

Pakua
Audio Credit
Anold Kayanda/Assumpta Massoi
Sauti
2'16"
Photo Credit
WFP/Souleymane Ag Anara