Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasema hali bado ni tete kwa watoto Cabo Delgado

UNICEF yasema hali bado ni tete kwa watoto Cabo Delgado

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema takribani watoto 250,000 wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia zinazoendelea kwenye jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji na sasa wako hatarini kupata magonwa ya kuambukiza kwa kuwa msimu wa mvua unaanza. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

 Hofu kubwa ya UNICEF ni kwamba huduma za kujisafi pamoja na maji safi na salama hazitoshelezi mahitaji yanayoongezeka ya watoto na familia zao kwenye kambi zao za muda ambamo wamejaa kupindukia.

“Huduma hizi lazima ziimarishwe haraka ili kuzuia mlipuko wa magonjwa yanayoenezwa kwa maji machafu kama vile kipindupindu halikadhalika ugonjwa wa Corona au COVID-19 ambao unahitaji uwepo wa maji safi na salama kwa ajili ya kunawa mikono,” imesema UNICEF.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietter Fore amenukuliwa katika taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo New York, Marekani na Maputo Msumbiji akisema kuwa katika kipindi kisichozidi miaka miwili, watoto na familia zao huko Cabo Delgado wamekumbwa na kimbunga, mafuriko, ukame, machungu ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na COVID-19 na sasa mapigano.

“Kadri hali inavyozidi kudorora Cabo Delgado, hasa wakati huu mvua zinapoanza, maji, huduma za kujisafi na mifumo ya afya inazidi kuzidiwa uwezo. Wadau wa kibinadamu walioko kwenye eneo hilo wanapaswa kuimarisha hizi huduma  ili kulinda uhai na ustawi wa watoto,” amesema Bi. Fore.

Watu wakiteka maji huko kambini Metuge jimboni Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji.
UNICEF/Mauricio Bisol
Watu wakiteka maji huko kambini Metuge jimboni Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji.

Bila maji safi, kipindupindu kitaleta hatari kubwa

Magonjwa yatokanayo na maji machafu kama vile Kipindupindu, ambayo yanaweza kuepukika na kutibiwa, yanaweza kusababisha vifo kwa watoto wakimbizi wa ndani iwapo watoto hao hawatopata maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi. Na hii ni dhahiri zaidi kwa watoto ambao tayari wana utapiamlo.

Watoto wawili kati ya watano jimboni Cabo Delgado wana utapiamlo na hiyo imechochewa zaidi na majanga yatokanayo  na hali ya hewa na mapigano.

Ukosefu wa chakula na njaa ndio matokeo ya hali hizo tete jimboni humo na sasa na watoto wengi zaidi wanabainika kuwa na utapiamlo uliokithiri.

UNICEF yachukua hatua

Kwa sasa UNICEF inapanua operesheni zake za kusambaza maji safi na huduma za kujisafi kwa kuziwezesha timu ambazo zinatembea nyumba kwa nyumba na makazi ya muda kupima hali ya utapiamlo kwa watoto na kuwapatia matibabu kama vile vyakula vyenye virutubisho halikadhalika chanjo.

Watoto wakimbizi wako hatarini zaidi kwa kuwa baadhi yao wamepoteza mawasiliano na familia zao na wanaweza kukabiliwa na ukatili wa kimwili au kisaiokolojia.

Baadhi ya watoto wameshuhudia ukatili, kama vile jamaa zao kuuawa mbele ya macho yao na sasa wanahitaji usaidizi wa kisaikolojia ili waondokane na kiwewe.

Tayari UNICEF imefungua vituo rafiki kwa watoto ambako watoto wakimbizi wanaweza kucheza salama na wataalamu wanabaini wale wanaohitaji msaada wa kisaikolojia.

Hata hivyo shirika hilo limesema kwa mwaka 2021 litahitaji dola milioni 52.8 ili kutekeleza operesheni zake za dharura za kibinadamu nchini Msumbiji, ambapo kati ya fedha hizo dola milioni 30 ni kwa ajili ya Cabdo Delgado pekee.

 

Audio Credit
Anold Kayanda/Jason Nyakundi
Audio Duration
1'54"
Photo Credit
UNICEF/Mauricio Bisol