Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Umoja wa Mataifa wakumbuka kusainiwa kwa Katiba yake

Mnamo Ijumaa Juni 26, hafla mbili tofauti ziliafanyika kuadhimisha miaka 70 tangu kusainiwa kwa Katiba ya Umoja wa Mataifa, ambayo kwayo, Umoja huo ulianzishwa. Hafla moja ilifanyika mjini San Francisco, jimbo la California, ambako katiba hiyo ilisainiwa mnamo Juni 26, mwaka 1945. Hafla ya pili ilifanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Katika Makala hii, Joshua Mmali anatumegea kidogo yaliyokuwemo katika matukio hayo.

Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani

Wakimbizi ni watu wa kawaida, kama mimi na wewe. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon aliuotoa wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya wakimbizi ambayo huadhimishwa Julai 20 kila mwaka. Bwana Ban ametaka kote duniani watu kuwavumilia kwa kuwaonyesha utu na kufungua mioyo kwa ajili ya wakimbizi.

Vijana changamkieni ubaharia #CareerAtsea: IMO

Ubaharia, taaluma ambayo kwa sasa inaonekana kuyoyoma na vijana wengi kuikwepa licha ya kuchangia kwa kiasi kikubwa katika biashara duniani. Takwimu za kiuchumi kutoka shirika la kimataifa la masula ya bahari, IMO zinasema kuwa asiilmia 90 ya biashara hiyo inatokana na bidhaa zinazosafirishwa kwa meli. Licha ya umuhimu huo, bado wafanyakazi wanaoshinda kutwa kucha kwenye meli hizo wakipitia safari za majini za muda mrefu bado ushujaa wao hautambuliki na idadi yao inapungua.

Picha: Benki ya dunia

Uchafuzi wa mazingira waanza kudhibitiwa Nigeria

Barani Afrika, miji inakumbwa na changamoto nyingi zitokanazo na kasi ya ukuaji wake.Benki ya Dunia inakadiria kuwa angalau miji nane barani Afrika itazidi idadi ya watu wanaoishi ya milioni 6, ikiwemo Nairobi, Kenya na Dar Es Salaam, Tanzania. Uchafuzi wa hewa, maji na ardhi huhatarisha afya ya binadamu na hatimaye ukuaji wa uchumi.

Nchini Nigeria, mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia umefanikiwa kuimarisha mwelekeo wa magari barabarani. Kulikoni ? Ungana na Priscilla Lecomte kwenye makala hii.

Haki ya ardhi kwa wakazi wa Hoima waliokumbwa na miradi ya visima vya mafuta

Nchini Uganda, harakati za kuanza kuchimba mafuta zimekuwa ni mwiba kwa baadhi ya wananchi ambao wanapaswa kupisha maeneo hayo kwa ajili ya miradi husika. Mathalani katika wilaya ya Hoima, mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta tayari umesabaisha kuhama kwa asilimia 90 ya wakazi waliokuwa wanapaswa kuondoka. Waliosalia bado kuna sintofahamu hususan ikizingatiwa umuhimu wa ardhi katika kaya za eneo hilo. Je nini kinafanyika, John Kibego kutoka Uganda anatuletea makala hii.

Utapiamlo ni miongoni mwa masaibu ya watoto wakimbizi kutoka Burundi

Mwezi mmoja baada ya mmiminiko wa kwanza wa zaidi ya wakimbizi 55,000 huko mkoani Kigoma,  Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, kufuatia hali ya shuka panda  ya kiusalama nchini Burundi. watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wako hatarini kuugua utapiamlo na wanahitaji msaada wa kibinadamu wa dharura. Habari hizo zinawekwa bayana wakati ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma ni watoto.Je hali ikoje? Ungana na Joseph Msami katika makala hii.

Harakati za kukabiliana na Kifua Kikuu sugu nchini Tanzania

Kifua Kikuu sugu, MDR-TB ugonjwa ambao unaendelea kuwa mwiba kwa watu 480,000 duniani kote, Tanzania ikiwa ni miongoni mwao. Shirika la afya duniani, WHO linasema kuwa MDR-TB ni ile ambayo ni sugu kiasi kwamba inagoma kutibika kwa dawa aina za isoniazid na rifampicin, ambazo yaelezwa ni tiba thabiti zaidi dhidi ya Kifua Kikuu. Sababu kuu za usugu ni matumizi mabaya ya dawa hizo wakati wa matibabu, mathalani wagonjwa kuruka siku za kupatiwa tiba au ubora duni wa dawa zenyewe.

Saksafoni yapunguza machungu ya ukimbizini

Kuelekea siku ya wakimbizi duniani tarehe 20 Juni mwaka huu wa 2015, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeweka bayana simulizi za wakimbizi kutoka maeneo mbali mbali duniani ambao kutwa kucha wanasaka maisha bora kule walikokimbilia huku taswira ya maisha ya nyumbani ikiendelea kusalia katika fikra zao. Miongoni mwa simulizi hizo ni ile ya Nader, mkimbizi kutoka Syria ambaye sasa anaishi Thailand.

Matumaini mapya kwa wahamiaji na wakimbizi walionusuriwa Mediterenia

Kufikia mwezi Juni, idadi ya wakimbizi na wahamiaji waliowasili Ulaya kupitia Bahari ya Mediterenia ni 112,000. Mnamo Jumanne, meli ya wanamaji wa Ireland iliwanusuru watu 400, na kuwapeleka kusini mwa Italia, ambako sasa wanapata usaidizi. Miongoni mwao, walikuwamo watoto na wanawake waja wazito.Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, wengi wa wahamiaji na wakimbizi hao walitoka kusini mwa jangwa la Sahara. Baadhi yao walikuwa wanatafakari kuhusu hatma yao, huku wengine wakiwa hawajui hatari ambazo wangekumbana nazo baharini.