Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Kweli nyumbani ni nyumbani: UNHCR

Wahenga walinena msahau kwao mtumwa, na nyumbani ni nyumbani hata iweje. Kauli hiyo si msemo tena bali ni hali halisi kwa maelfu ya wakimbizi wa Kisomali walioamua kuchukua hatua ya kurejea nyumbani baada ya kuishi kwa miaka mingi kwenye makambi ya wakimbizi ya Dadaab na Kakuma nchini Kenya. Flora Nducha na taarifa kamili.

Natts……

MONUSCO yajenga uwezo polisi kuelekea uchaguzi mkuu DRC

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO unaendesha mafunzo ya kujengea uwezo wasimamizi wa uchaguzi pamoja na polisi nchini humo wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.

Mkuu wa kitengo cha polisi, MONUSCO Kamishna Mkuu Awalé Abdounasir, amesema mafunzo hayo yanayofanyika kwenye mji mkuu Kinshasa, yanalenga kuhakikisha polisi wanazingatia sheria na kanuni wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Dola bilioni 1.7 zahitajika kusaidia wananchi wa Sudan Kusini

Mzozo nchini Sudan Kusini ukiingia mwaka wa nne, zaidi ya dola bilioni 1.7 zahitajika ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu kwa nchini humo kwa mwaka 2018.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini humo Alain Noudéhou ametangaza kiwango hicho hii leo kwenye mji mkuu, Juba akisema mpango huo unalenga watu milioni 6 walioathiriwa zaidi na mzozo, kupoteza makazi, njaa na kudorora kwa uchumi.

Taka za kielektroniki zasalia kwenye makabati majumbani- Ripoti

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imebaini ongezeko kubwa la taka za kielektroniki ulimwenguni.

Taka hizo ni pamoja na betri chakavu, plagi za umeme, majokofu, simu za kiganjani na kompyuta ambazo kiwango chake mwaka 2016 kilifikia tani za ujazo milioni 44.7.

Kiwango hicho ni ongezeko kwa asilimia 8 ikilinganishwa na mwaka jana na mwelekeo ni ongezeko zaidi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuporomoka kwa bei za vifaa vya kielektroniki na umeme na hivyo kuwa kishawishi kwa watu kununua vifaa vipya na kutupa hovyo vya zamani.

Ukimpa mwanamke fursa, jamii itanufaika

Kuna usemi wa kwamba ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii na ukielimisha  jamii basi utakua umeokoa  kizazi cha baadaye. Huu usemi  hauna maana ya upendeleo bali  ni ukweli kwamba ukimpa mwanamke fursa basi  jamii itanufaika zaidi. Hii inatokana na mapenzi, malezi, na moyo wa ujasiri aliojaliwa  mwanamke.

Madhila dhidi ya raia yaongezeka mzozoni Ukraine; UM

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa leo inasema madhila dhidi ya raia katika mzozo wa kivita nchini Ukraine huenda yakaongezeka zaidi, kufuatia kuibika upya kwa mapigano.

Ripoti hiyo inasema mapigano hayo yameathiri watu milioni nne nukta nne kwa sasa, yakisababisha vifo zaidi na uharibifu mpya kwa miundombinu muhimu ya maji inayohifadhi kemikali hatari, kinachotishia uhai wa binadamu na mazingira.

Haya yote yakitokana na ukiukwaji wa mara kadhaa wa mikataba ya kusitisha mapigano.

Kuwekeza kwenye Malaria ni hatua chanya- Dkt. Winnie

Uwekezaji katika kukabiliana na Malaria, ni uwekezaji ambao utasaidia siyo tu kutokomeza umaskini bali pia kuchochea maendeleo kwa ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Dkt. Winnie Mpanju Shumbusho, ambaye ni mwenyekiti wa ubia wa kutokomeza Malaria duniani, RBM amesema hayo katika mahojiano maalum na Idhaa hii akisema kuwa..

(Sauti ya Dkt. Winnie Mpanju Shumbusho)

Amesema hata nchi ambazo hivi sasa hazina Malaria zilikuwa na ugonjwa huo lakini zilichukua hatua akitolea mfano Marekani.