Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa haki waongeza sauti kwenye suala la utoweshwaji wa watu

Wataalamu wa haki waongeza sauti kwenye suala la utoweshwaji wa watu

Pakua

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa na wa kanda mbalimbali ikiwemo Afrika na Asia wameyasihi mataifa yote kutoa haki kwa waathirika wa utoweshwaji wa watu, ikiwa ni pamoja na mtu yeyote ambaye amepata madhara kama matokeo ya moja kwa moja ya utoweshwaji wa watu. Anold Kayanda na maelezo zaidi. 

"Kuhakikisha haki ya waathiriwa kunahitaji kuchukua hatua zote muhimu ili kufichua ukweli," wataalam hao wamesema katika taarifa walioitoa jana mjini Geneva, Uswisi kuelekea leo ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Waathiriwa wa Kutoweshwa kwa watu.  

Wataalamu hao wanasema kwamba kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa haki na uwajibikaji ipasavyo kwa wahalifu katika ngazi zote za mnyororo mzima wa amri ni muhimu ili kuwasilisha ujumbe mzito kwamba kutowesha watu ni uhalifu chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, hairuhusiwi au kuvumiliwa. 

Kwa mujibu wa Azimio la Ulinzi wa Watu Wote dhidi ya Kutoweshwa kwa Watu, lililotangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika azimio lake la 47/133 la tarehe 18 Desemba 1992 kutoweshwa ni pindi "Watu wanakamatwa, kuwekwa kizuizini au kutekwa nyara bila hiari yao au kunyimwa uhuru wao kwa njia nyingine na maafisa wa matawi au ngazi mbalimbali za Serikali, au na makundi yaliyopangwa au watu binafsi kwa niaba ya, au kwa msaada, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ridhaa au kukubaliana na Serikali, ikifuatiwa na kukataa kufichua hatima au mahali walipo watu waliokamatwa au kukataa kukiri kunyimwa uhuru wao, jambo ambalo linawaweka watu hao nje ya ulinzi wa sheria." 

Wataalamu wa haki za binadamu wanasema "Katika mapambano yao ya kila siku ya haki, waathiriwa mara nyingi wanakabiliwa na vitisho, kisasi na unyanyapaa. Hili lazima likomeshwe, na waathiriwa lazima wapate msaada wa kisheria bila malipo ili kuhakikisha kuwa hali yao ya kifedha haiwazuii kutafuta haki na upatikanaji wa haki lazima usiwe wa kinadharia tu bali uhakikishwe kivitendo kupitia hatua madhubuti zinazokuza na kuthamini kikamilifu ushiriki wa kweli na wa maana wa waathiriwa na wawakilishi wao katika mchakato wote."  

Audio Credit
Assumpta Massoi/Anold Kayanda
Audio Duration
2'20"
Photo Credit
Centro de Estudios Ecunémicos