Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa "Njoo shuleni" nchini Kenya warejesha matumaini kwa familia

Mradi wa "Njoo shuleni" nchini Kenya warejesha matumaini kwa familia

Pakua

Elimu ni moja ya nyenzo zenye nguvu zaidi za kuleta mabadiliko kwa watu binafsi na jamii na ndio maana katika miongo miwili iliyopita, serikali ya Kenya imefanya mageuzi mengi ili elimu ya msingi iwe bure na ya lazima kwa watoto wote walio katika umri wa kwenda shule. 

Hata hivyo, watoto wengi bado hawako shuleni kutokana na umaskini, miundombinu duni, kutelekezwa na wazazi na matatizo ya kiafya hasa katika maeneo masikini. Sasa shirika la Umoja la kuhudumia watoto UNICEF limeamua kuingilia kati kwa kushirikiana na wadau kusaidia. Flora Nducha na maelezo zaidi.

Katika Kaunti ya Dandora jijini Nairobi ambako wakazi wengi ni walala hoi, watoto kwenda shule ni mtihani unaoanzia kwa wazazi kama Wambui Kahiga mama wa Octavia mtoto mwenye umri wa miaka 10.

Wambui anasema, “shida zangu kubwa sasa hivi ni chakula, mavazi , kulipa gharama za shule na ghara za kulipia nyumba. Kibarua ninachopata wakati huu ni cha kufua nguo na hakiaminiki kuna wakati napata na kuna wakati nakosa. Najihisi vibaya kwani ingekuwa mapenzi yangu , Octavia angekuwa alianza shule kitambo.”

Kwa mujibu wa UNICEF umasikini ndio sababu kubwa inayowafanya wazazi kushindwa kuwapeleka watoto shule na sasa shirika hilo linashirikiana na wakfu wa Elimisha mtoto (EAC) na wanaendesha programu ya elimu zaidi ya yote kupitia mradi wa “Njoo shuleni” ili kuwafikia watoto wote kama Octavia na kuhakikisha wanapata haki ya elimu.

Elizabeth Waitha ni afisa elimu wa UNICEF Kenya anasema “mara tunapobaini watoto ambao hawana fursa ya elimu, tunawasajili na tunaweza kuwasaidia na vifaa vya shule ambavyo vinapunguza mzigo kwa wazazi kuweza kuwasaidia watoto wao kwa ajili ya kusoma”.

Na hii inaleta faja na matumaini kwa watoto na wazazi kama kwa mama wa Octavia akisema, “Octavia yuko shuleni , na sasa ambavyo anasoma naona maisha yake yatabadilika , yatakuwa maziri hata mimi atakuja kuniinua.”

Kwa UNICEF “Elimu ni haki ya msingi ya binadamu na kila mtoto anapaswa na anahitaji fursa ya kupata elimu na uelimishaji mkubwa unahitajika kuhakikisha kwamba kila mtoto anasoma.”

Kulingana na takwimu za Educate A Child (EAC) kuna watoto milioni 1.3 wa umri wa kati ya miaka 6 hadi 13 ambao hawasomi nchini Kenya.

Mradi huu unafadhiliwa na mfuko kwa ajili ya maendeleo wa serikali ya Qatar na unatekelezwa katika kaunti 16 nchini Kenya ambazo ni Baringo, Bungoma, Garissa, Isiolo, Kajiado, Kilifi, Kwale, Mandera, Marsabit, Narok, Samburu, Tana River, Turkana, Wajir, West Pokot, na katika makazi yasiyo rasmi ya jijini Nairobi.

Audio Credit
Leahj Mushi/Flora Nducha
Audio Duration
2'53"
Photo Credit
UNICEF Kenya/2023/Translieu