Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa Tanzania watoa msaada nchini CAR

Walinda amani wa Tanzania watoa msaada nchini CAR

Pakua

TANBAT-5 waanza mwaka mpya kwa kutembelea gereza CAR na kutoa msaada
Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, kikosi cha 5 cha Tanzania, TANBAT-5 kinachohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MINUSCA kimefungua mwaka 2022 kwa kutembelea gereza la wafungwa lililoko wilaya ya Berberati, mkoa wa Mambere Kadei, eneo ambalo ni makao makuu ya kikosi hicho, ikiwa ni kitendo cha ukarimu kwa wafungwa hao.

Taarifa zaidi na Kapteni Asia Husseni, Afisa Habari wa TANBAT-5

Katika ziara hiyo, TANBAT-5 ilipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya gereza hilo na kujionea shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo cha bustani za mboga mboga, utengenezaji mikoba, samani za majumbani na ufyatuaji wa matofali.

Msimamizi wa gereza hilo Bemonza Ferdina kupitia mkalimani, amewashukuru TANBAT-5 kwa ushirikiano wanaonesha na kuomba uendelee kwa siku zote hadi amani ya nchi hiyo itakapotengamaa.

“MINUSCA Berberati siku zote tuko nao pamoja na tunafurahishwa na kuendelea kuwa pamoja. Na MINUSCA Tanzania pia imekuwa inatusaidia kila siku na tunafurahishwa na hilo. Na mahusiano haya yanatakiwa yaendelee mpaka mwisho. Siku zote tuko pamoja na ni kwa wema wa MINUSCA ndio maana mpaka sasa hivi tumefikia hapa tuliko na mambo ni mazuri.”

Bwana Ferdina ameongeza kuwa amefurahishwa na utamaduni wa vikosi vya Tanzania tangu kikosi cha kwanza kilipofika nchini humo, kwani vimekuwa mstari wa mbele kujitoa kwa ajili ya raia nchini humo.

Naye Kapteni Abdalla Salehe, kwa niaba ya mkuu wa kikosi cha TANBAT-5 amemhakikishia msimamizi wa gereza hilo kuwa ushirikiano huo utaendelea kwa kuwa si sehemu tu ya utekelezaji wa majukumu  yao bali pia ni kujali utu na ubinadamu.

Audio Credit
Assumpta Massoi /Kapteni Asia Husseni
Audio Duration
2'17"
Photo Credit
MINUSCA/Catianne Tijerina