Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Waliofurushwa makwao Iraq wahaha kwa mapigano zaidi na baridi

Watu wapatao 400,000 nchini Iraq hawana makazi ya kutosha huku wengine 780,000 wakiishi bila bidhaa muhimu za nyumbani na za kuendeleza ubora wa maisha yao wakati huu wa msimu wa baridi kali, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA.

Kwa mujibu wa OCHA, serikali ya Iraq na wadau wa kitaifa na kimataifa wanaoa usaidizi wa vifaa vya kupasha moto mahema, nguo za joto, fedha, mafuta na vifaa vingine vya kuboresha hali ya maisha.

Karen AbuZayd ndiye mshauri wa mkutano wa masuala ya wakimbizi na wahamiaji

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ametangaza leo uteuzi wa Bi Karen AbuZayd wa Marekani kama mshauri maalumu wa mkutano wa kushughulikia wimbi kubwa la uhamaji wa wakimbizi na wahamiaji ambao utafanyika kwenye baraza kuu la umoja wa Mataifa mwezi septemba 2016.

Mshauri huyo maalumu atafanya kazi kwa karibu na vyombo vya Umoja wa Mataifa na kufanya mashauriano nan chi wanachama na wadau wengine hadi wakati wa mkutano huo.

Safari kuelekea mlima Kilimanjaro kwa ajili ya amani

Walinda amani kutoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS katika juhudi za kueneza ujumbe wa amani ulimwenguni na nchini Sudan Kusini walipanga safari kuelekea nchini Tanzania kwa lengo la kupanda mlima Kilimanjaro ili kupandisha bendera ya Umoja wa Mataifa katika kilele cha mlima huo. Safari hii ambayo ni ya kwanza kuwahi kufanyika miongoni mwa walinda amani ilitimia pale ambao bendera ya Umoja wa Mataifa ilipepea kileleni.Ungana na Grace Kaneiya  katika makala ifuatayo.

Ban alaani mashambulizi dhidi ya magari ya vikosi vya Israel

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi ya jana dhidi ya magari mawili ya vikosi vya julinzi vya Israel katika eneo la mashamba ya Sheba’a mashambulizi ambayo Hizbullah imedai kuhusika.

Katibu Mkuu ameelezea hofu yake dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ya vikosi vya Israel kusini mwa Lebanon , eneo ambalo vikosi vya mpango wa Umoja wa mataifa nchini Lebanon UNIFIL vinaendesha operesheni zake.

Wibisono azungumzia kisa cha kung’atuka ufuatiliaji suala la Palestina

Mtaalamu  maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu kwenye maeneo ya wapalestina, Makarim Wibisono amezungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu wadhifa huo ifikapo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huu.

Wibisono amesema msingi wa hatua hiyo ni kitendo cha Israeli kumnyima haki ya kutembelea maeneo yanayokaliwa ya wapalestina akisema harakati zake za kuboresha maisha ya wapalestina ambao haki zao zinakandamizwa zimekatishwa tamaa kila mara.

Watu 9 wafariki dunia katika tetemeko la ardhi India na Bangladesh

Watu wapatao tisa wameripotiwa kufariki dunia leo Jumatatu Januari 4, kufuatia tetemeko la ardhi lililolikumba jimbo la Manipur nchini India, na kuathiri pia nchi jirani za Bangladesh na Myanmar, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA.

Miongoni mwa walioripotiwa kufariki dunia katika tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.7 kwenye kipimo cha richa, ni watu wanane nchini India na mtu mmoja nchini Bangladesh, huku watu zaidi ya 100 wakiripotiwa kujeruhiwa, hususan kwa maporomoko ya nyumba karibu mji mkuu wa jimbo la Manipur, Imphal.

UM walaani mashambulio dhidi ya misikiti Babylon Iraq

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Iraq Ján Kubiš, amelaani mashambulio yaliyofanyika dhidi ya misikiti mitatu ya Kisuni kwenye jimbo la Babylon usiku wa kuamkia leo na vitendo vingine vya ghasia.

Mashambulio hayo matatu ni jarikbio la kuongeza mvutano nchini Iraq na kwenye ukanda mzima amesema bwana Kubiš.Akiongeza kwamba walioendesha mashambulizi hayo wanajaribu kutumia hali ya sasa ya kikanda na kudhoofisha umoja wa Iraq na watu wake na wanatimiza matakwa ya magaidi wa ISIL.

Waliojitokeza kushiriki uchaguzi wa CAR ni 75%- MINUSCA

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA umeripoti kuwa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi ANE imetangaza baadhi ya matokeo ya uchaguzi siku ya Jumapili hii kulingana na kura zilizopigwa kwenye majimbo nane na asilimia 15 ya kura zilizopigwa nje ya nchi.

Hii ni kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric ambaye amewaambia leo waandishi wa habari mjini New York Marekani kwamba matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa mwisho wa wiki hii na kuthibitishwa na Mahakama ya Kikatiba tarehe 15 Januari.

UN Photo/NICA

Ban amezungumza kwa simu na mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya nje wa Saudia Abel bin Ahmed Al-Jubeir, na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif.

Akizungumzana Bwana Zarif, Ban amerejea kauli yake kuhusu mauaji ya Sheikh al-Nimr na wafungwa wengine 46 yaliyotekelezwa na serikali ya Saudia Januari pili mwaka huu. Pia amezungumzia kulaani kwake vikali shambulizi dhidi ya ubalozi wa Saudia mjini Tehran na amemtaka waziri huyo wa mambo ye nje kuchukua hatua zinazohitajika kulinda maeneo ya kidplomasia nchini humo.

Somalia yaaga Nicholas Kay, aliyeitwa rafiki wa kweli

Aliyekuwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja huo nchini Somalia Nicholas Kay amehitimisha hivi karibuni muda wake kwenye nafasi yake.

Zaidi ya miaka miwili imepita tangu alipofika mjini Mogadishu mwezi Juni mwaka 2013 na viongozi wa Somalia pamoja na wafanyakazi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM wameandaa hafla maalum kwa yule aliyetajwa kuwa rafiki wa ukweli wa Somalia.

Kwa mengi zaidi kuhusu hafla hiyo, ungana na Priscilla Lecomte kwenye makala hii.