Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inaonya kwamba njaa inaongezeka Gaza hakuna chakula wala nishati ya kupikia na kukaribisha magonjwa zaidi

WHO inaonya kwamba njaa inaongezeka Gaza hakuna chakula wala nishati ya kupikia na kukaribisha magonjwa zaidi

Pakua

Njaa imeukumba Ukanda wa Gaza kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na hivyo kutishia ongezeko la magonjwa hususan miongoni mwa watoto, kina mama wajawazito na wanaonyonyesha na makundi mengine yaliyo hatarini na nishati ya kupikia nayo imeota mbawa. 

Majira ya mchana mlo unandaliwa katika eneo la Rafah kwa ajili ya wakimbizi wa ndani wakishuhudia kwa hamu kubwa na zana zao mikononi mabakuli , vikombe na hata masufuria. Mlo wenyewe ni uji unaopikwa katika masufuria makubwa na kwa ukosefu wa gesi unapikwa kwenye kuni ambazo sasa ni adimu na ndio nishati pekee inayotegemewa.

WHO inaonya kwamba Gaza inakabiliwa na viwango vikubwa vya ukosefu wa chakula na kila siku kuwa hatarini kukumbwa na baa la njaa. Watu hawa hawana chochote kama anavyoema mmoja wa wapishi ambaye pia ni mkimbizi wa ndani,“Vita hii imetudhalilisha kwa kiwango kisichoelezeka, Tunataabika na kudhalilika ili tu tupate mmlo wa mchana. Maisha hapa yamekuwa ghali sana hatuwezi kumudu, hatuli, hatunywi wala kulala vizuri na hakuna kinachopatikana.”

Uji sasa tayari na unaanza kugawiwa, mwenye kikombe, mwenye bakuli haya ili mradi kila mtu anagombea maana huenda huu ndio mlo pekee atakaoupata kwa siku hii watu ni wengi. Mpishi huyu anaongeza, “Inachukua dadika 45 kwenda kwa mguu kufuata chakula hii na dakika 45 zingine kurudi ili nipike na kuwagawia , sijui nisema nini zaidi , hali ni ngumu sana.”

Katika baadhi ya mitaa ya Rafah kuna vitu vichache vinavyouzwa kama vile vyakula vya makopo na barabarani kina mama na baba lishe wanajitahidi kupika wakipatacho na kuuza. Mkimbizi huyu wa ndani aliyekuja kununua chakula hicho anasema “Leo hii tuko katika hali mbya sana kwenye makazi ya muda, kuna vurugu, machafuko na mambo yasiyowezekana, sisi si watu wabaya , hata msaada wa chakula unaotolewa na UNRWA na mashirika mengine ni gharama kuuandaa na kupika kuliko hata thamani yake. Watu hawawezi kununua au kuandaa chakula kutokana na ukosefu wa gesi.”

Wakimbizi hawa wa ndani wanasema watoto wao wengi sasa ni wagonjwa wana mafua, kukohoa matatizo ya tumbo na huduma ni haba. Mafuta pia hayapatikani  wenye magari sasa wakilazimika kujaza matanki yao kwa mabaki ya mafuta ya kupikia  na si salama kwa afya zao.

Kwa mujibu wa WHO kuna wagonjwa zaidi ya 100,000 wa kuhara Gaza tangu katikati ya Oktoba na nusu yao ni watoto wa umri wa chini ya miaka 5 na pia kuna wagonjwa zaidi ya 150,000 wa magonjwa ya mfumo wa hewa, lakini pia uti wa mgongo, upele, wenye chawa na tetekuanga.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
© WFP/Mostafa Ghroz