Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko waliofanikisha sitisho la mapigano Gaza - Guterres

Heko waliofanikisha sitisho la mapigano Gaza - Guterres

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezipongeza serikali za Qatar, Misri na Marekani pamoja na kutambua jukumu muhimu la kamati ya Kimataifa ya chama cha msalaba mwekudu kwa juhudi zao za kuhakikisha mapigano yanasitishwa kwa muda, mateka na wafungwa wanaachiwa pamoja na kuingiza misaada huko Ukanda wa Gaza. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Flora Nducha

Mapigano ya wiki saba huko Gaza na Israel yameleta hali mbaya sana ambayo imeshangaza ulimwengu. Lakini kwa muda wa siku nne sasa, Mapigano hayo yamesitishwa, Mateka wa Israel na mataifa mengine ya kigeni wanaoshikiliwa na Hamas tangu tarehe 7 Oktoba wameanza kuachiliwa na wafungwa wa Kipalestina wanafunguliwa kutoka jela za Israel.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia Msemaji wake Stéphane Dujarric hii leo hapa jijini New York Marekani amewapongeza wahusika wote walioshiriki kufanikisha hayo yanayoendelea kutokea.  

Umoja wa Mataifa pia umeongeza uingizaji misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na misaada mingine imetumwa eneo la kaskazini mwa Gaza ambalo kwa wiki kadhaa wananchi waliokosa misaada kutokana na mapigano makali yaliyoendelea katika eneo hilo.

Hata hivyo Katibu Mkuu Guterres amesema misaada hiyo haitoshi kukidhi mahitaji ya wananchi milioni 1.7 wenye uhitaji na kusema mahitaji ya kibinadamu kila uchao yanazidi kuongezeka.

Ametaka mazungumzo yaliyokuwa chachu ya makubaliano hayo lazima yaendelee, na kufikia usitishaji kamili wa mapigano kwa sababu za kibinadamu, kwa manufaa ya watu wa Gaza, Israel na eneo zima.

Katibu Mkuu kwa mara nyingine ametoa wito kwa mateka waliosalia kuachiwa mara moja bila masharti yoyote.

Amehitimisha taarifa yake kwa kuyahimiza Mataifa yote kutumia ushawishi wao kumaliza mzozo huu mbaya na kuunga mkono hatua zisizoweza kutenguliwa kuelekea mustakabali pekee endelevu wa eneo hilo ambao ni suluhisho la kuwa na serikali mbili, na Israeli na Palestina kuishi bega kwa bega, kwa amani na usalama.

Wakati huo huo wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa hii leo wametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka, wa uwazi na huru kuhusu tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, unaotekelezwa nchini Israel na katika eneo linalokaliwa la Palestina kuanzia tarehe 7 Oktoba mwaka huu wa 2023 na baada ya hapo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi imesema wataalamu hao wamezitaka pande zote katika mzozo unaoendelea huko Mashariki ya Kati kuwalinda raia na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa.

Audio Credit
Leah Mushi/Flora Nducha
Audio Duration
2'40"
Photo Credit
© UNICEF/Abed Zaqout