Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS wataka wanasiasa Sudan Kusini wapatie wanachi elimu ya kisiasa

UNMISS wataka wanasiasa Sudan Kusini wapatie wanachi elimu ya kisiasa

Pakua

Wakati nchi ya Sudan Kusini ikijiandaa kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza kabisa tangu ipate uhuru, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS unaendesha makongamano na vyama vya siasa nchini humo. 

Ikiwa imesalia miezi 15 mpaka uchaguzi ufanyike hapo Desemba 2024 UNMISS wanasema lengo la kuandaa makongamano hayo nikujenga utamaduni wa kuwa na mazungumzo thabiti, kutatua changamoto zinazowakabili kuhusu utawala bora na kujenga kuaminiana miongoni mwa wanasiasa na jamii wanazozitumikia. 

Akiwa katika moja ya majukwaa huyo katika mji mkuu wa Juba Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ambaye pia ni Mkuu wa UNMISS, Nicholas Haysom aliwaambia washiriki kuwa, “Uchaguzi hauwezi kufanyika ikiwa hakuna makubaliano ya masuala ya kiufundi. Hisia za uharaka walizonazo jumuiya ya kimataifa kuhusu uchaguzi hazisaidii. Udharura unawahusu Wasudan Kusini — wananchi, na hasa vyama vya siasa, ndiyo maana tutawaomba nyinyi kufanya kazi na kutusaidia sisi katika kuunda na kuelewa asili ya chaguzi mnazotaka kufanya ili na sisi tuweze kuhamasisha kupatikana kwa misaada kwa ajili ya mambo hayo.”

Si wanasiasa pekee wanaohudhuria makongamano hayo bali pia wasomi ambao wamehimiza umuhimu wa kuwa na ushiriki mkubwa wa umma katika michakato ya amani, pamoja vyama vya siasa kuwa na ushindani imara kama anavyoeleza Adwak Nyaba, “Vyama vya siasa vinapaswa kuhimiza elimu ya kisiasa ili kuongeza ufahamu wa kijamii na ufahamu wa kisiasa wa wananchi. Ni kutokana na kuwepo kwa ufahamu wa kisiasa na watu wanaozingatia siasa kunakowezesha uwepo wa serikali za kidemokrasia. Ikiwa watu hawana ufahamu kabisa wa kisiasa, huwezi kuzungumzia utawala wa kidemokrasia, au huwezi kuzungumzia demokrasia.”

Wanasiasa wamehimizwa kufikia makubaliano ya masuala muhimu haswa kuhusu uanzishwaji wa taasisi muhimu ambazo ni Baraza la Vyama vya Siasa, Tume ya Kitaifa ya Marekebisho ya Katiba na Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi.

Audio Credit
Leah Mushi
Sauti
2'21"
Photo Credit
UNifeed Video