Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya uchaguzi mkuu Zimbabwe Guterres aomba amani

Baada ya uchaguzi mkuu Zimbabwe Guterres aomba amani

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema anafuatilia kwa karibu kinachoendelea kwenye mchakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Zimbabwe tarehe 23 mwezi huu wa Agosti. 

Taarifa iliyotolewa Jumapili jioni na ofisi ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inasema Katibu Mkuu Guterres katika ufuatiliaji wa kinachoendelea nchini humo, hofu yake kubwa ni ripoti za kukamatwa kwa waangalizi wa uchaguzi, vitisho dhidi ya wapiga kura, vitisho vya ghasia, halikadhalika manyanyaso na matumizi ya nguvu.  

Hofu ya Guterres inakuja wakati ambapo tayari vyombo vya habari vinaripoti kuwa Rais wa sasa Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa ameibuka na ushindi kwenye kinyang’anyiro cha urais kilichokuwa kinawaniwa na wagombea 11.  

Katibu Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kuepuka aina yoyote ya ghasia au kuchochea ghasia, na badala yake wahakikishe haki za binadamu na utawala wa sheria vinaheshimiwa.    

Ametoa wito pia kwa washiriki wote kwenye siasa kutatua mizozano yoyote ile kupitia njia za kisheria na taasisi zilizowekwa kwa ajili hiyo.  

Bwana Guterres amezitaka taasisi husika zitatue migogoro yoyote itakayoibuka kwa njia ya haki, uwazi na haraka ili kuhakikisha matokeo ya uchaguzi huo yanaakisi utashi wa wananchi wa Zimbabwe.  

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa wagombea kutoka upinzani wamekataa matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi Rais Mnangagwa kwa asilimia 52.6, matokeo yaliyotangazwa Jumamosi na Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe.  

Bwana Mnangagwa aliingia madarakani kufuatia uchaguzi wa mwaka 2018. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'35"
Photo Credit
© Brent Stirton/Getty Images for FAO