Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO, UNWTO: Utalii milimani unaweza kuimarisha baiyonuai na vipato vya wakazi wa maeneo hayo

FAO, UNWTO: Utalii milimani unaweza kuimarisha baiyonuai na vipato vya wakazi wa maeneo hayo

Pakua

Ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau imeeleza bayana jinsi utalii kwenye maeneo ya milimani unaweza kuwa na manufaa sio tu kwa baiyonuwai bali pia kwa jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo.

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO mjini Roma, Italia hii leo imesema chapisho hilo limetolewa ili kwenda sambamba na hitimisho la mwaka wa kimataifa wa maendeleo endelevu ya milima ulioanza mwaka jana wa 2022. 

Chapisho hilo linasema utalii wa milimani iwapo utasimamiwa kwa uendelevu, una nafasi kubwa ya kuinua vipato vya jamii zinazozingira maeneo hayo na kusaidia kulinda maliasili na utamaduni. 

Hata hivyo imebainika kuwa ukosefu wa data na ufahamu kuhusu fursa za kiuchumi na mazingira zitokanazo na utalii wa milimani umezuia jamii nyingi kunufaika na fursa hizo. 

FAO kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la utalii duniani, UNWTO na shirika la Mountain Partnership, MP, wametoa ripoti hiyo kama njia ya kuondoa pengo ili hatimaye jamii za maeneo ya milimani zipate kunufaika na fursa zilizoko. 

Mathalani chapisho linataka kusongesha upatikanaji wa takwimu za utalii wa milimani ambako ni makazi ya watu wapatao bilioni 1.1, baadhi yao wakiwa ni wale hohehahe zaidi na waliotengwa. 

Milima ina maeneo ambako watalii wanaweza kutembea, kupanda na kufanya michezo nyakati za majira ya baridi kali. Maeneo hayo yanaweza pia kuvutia wageni kutokana na taswira zake, utajiri wa  baiyonuai na tamaduni za kipekee. 

Hata hivyo takwimu za karibuni zaidi za mwaka 2019 zinaonesha nchi 10 zenye milima zaidi duniani zilipokea asilimia 8 pekee ya watalii wa kimataifa duniani kote. 

Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu na Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololikashvili kupitia utangulizi wa ripoti hiyo wamesema kupata takwimmu za watalii wa milimani ni hatua ya kwanza muhimu tunayopaswa kuchukua. Uwepo wa takwimu sahihi utawezesha kufuatilia mienendo ya utalii kwenye maeneo hayo na kisha kutumia takwimu kusaidia mipango na kuandaa bidhaa endelevu kulingana na mahitaji ya watalii kwenye kila eneo husika na hatimaye sera za kuchochea utalii wenye manufaa kwa jamii. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
2'11"
Photo Credit
©WTO