Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Upper Nile yasababisha wakimbizi wengi wahame makwao nchini Sudan Kusini.

Mapigano Upper Nile yasababisha wakimbizi wengi wahame makwao nchini Sudan Kusini.

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema limesikitishwa na kuongezeka kwa mapigano katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini ambayo umesababisha takriban watu 20,000 kuyahama makazi yao tangu mwezi Agosti, baadhi yao wakilazimika kukimbia hadi mara nne ili kuokoa maisha yao huku mzozo huo ukiendelea. 

Kwa mujibu wa taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis na Juba Sudan takriban watu 3,000 tayari wamekimbilia nchi jirani ya Sudan, na hivyo kuzidisha mzozo wa wakimbizi wa Sudan Kusini, ambao ndio mkubwa zaidi barani Afrika. 

Mapigano yalizuka katika kijiji cha Tonga huko Upper Nile tarehe 15 Agosti 2022. Ghasia zimeenea zaidi katika jimbo la Upper Nile, sehemu za kaskazini za Jonglei na majimbo ya Unity na machafuko yanasambaa sasa katika kaunti ya Fashoda ya Upper Nile na kutishia mji wa Kodok. 

Mwakilishi wa UNHRC nchini Sudan Kusini Arafat Jamal amesema “Taharuki inaongezeka na watu zaidi wanakimbia wakati machafuko yakishika kasi. Raia wanashambuliwa katika mgogoro huu usio na huruma lazima tuhakikishe ulinzi wao.” 

Ameongeza kuwa wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika hatari kubwa ndio idadi kubwa ya waliotawanywa na baadhi ya wazee na watu wenye ulemavu wameshindwa kukimbia na kulazimika kujificha porini na kando yam to Nile wakati wa mashambulizi. 

Kwa raia wanaokimbia UNHCR inasema ni “Dhahiri wameathirika na wameripoti mauaji, majeruhi, ukatili wa kijinsia, watu kutekwa, uporaji, unyang’anyi na uchopaji wa mali huku wengi wakisema wamepoteza nyumba zao na kutengana na familia zao.” 

Wakati huohuo jumuioya ya kibinadamu nchini Sudan Kusini imelaani vilaki kuendelea kwa machafuko hayo na kaimu mratibu wa masuala ya kibinadamu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada yad harira OCHA Peter Van der Auweraert akisistiza kwamba "Jumuiya ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inasikitishwa na ghasia zinazoendelea ambazo zina athari mbaya kwa uwezo wa watu kuishi na maisha ya wanawake wa kawaida, wanaume na watoto na wale walio hatarini ambao tayari wameathiriwa na hali mbaya ya kibinadamu nchini humo ndio wanaoteseka zaidi.” 

Hivi sasa UNHCr na wadau wanaongeza juhudi za msaada wa kibinadamu na kuwafikia hata walio maeneo ya vijijini zaidi.  

“Watu milioni 6.8 Sudan Kusini wanahitaji haraka msaada wa kuokoa maisha kutokana na changamoto mchanganyiko ikiwemo vita, mafuriko, kutokuwepo uhakika wa chakula na kuyumba kwa uchumi.” 

Na ombi la UNHCR la usaidiazi kwa taifa hilo mwaka 2022 la dola milioni 214.8 hadi kufikia Novemba mwaka huu lilikuwa limefadhiliwa kwa asilimia 46 pekee. 

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
2'57"
Photo Credit
© UNHCR/Charlotte Hallqvist