Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lt. Jenerali Tinaikar - Walinda amani wanawake wanafanya wanafanya kazi nzuri

Lt. Jenerali Tinaikar - Walinda amani wanawake wanafanya wanafanya kazi nzuri

Pakua

Luteni Jenerali Shailesh Tinaikar raia wa India ambaye anastaafu wadhifa wake kama Kamanda wa Kikosi cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS amewashukuru askari walinda amani waliokuwa chini yake hususani wanawake ambao anasema wanafanya kazi katika mazingira yenye changamoto zaidi. John Kibego anaeleza zaidi.

Ni Luteni Jenerali Shailesh Tinaikar akikagua gwaride la wanajeshi walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliosimama kikakamavu.  

Luteni Jenerali Shailes Tinakar anasema ingawa alijiunga jeshini kinyume na mapenzi ya wazazi wake, lakini hakuwahi kuwaza kingine zaidi ya kuwa mwanajeshi na kupitia jeshini ameihudumia dunia kwa ngazi mbalimbali jeshini nchini mwake akipanda vyeo vya juu, kanali, Brigedia, Meja Jenerali na baadaye kuhudumu katika Umoja wa Mataifa kama Mkuu wa Kikosi UNMISS akiwa Luteni Jenerali.  

Katika miaka yake ya kuhudumu kwenye UNMISS, Kamanda wa Kikosi Tinaikar amejenga uhusiano wa kuaminiana na watu wa Sudan Kusini, akizishinda changamoto zinazoletwa vurugu na hata ugonjwa wa Covid-19 ukimlazimisha kubadili kwa kiasi fulani utaratibu wa kawaida wa operesheni za UNMISS. "Kuna watu walikufa hapa, na miili yao haikuweza kurejeshwa kwa wakati. Kwa hivyo, mtu ulihisi hali ya huzuni katika kipindi hiki. Lakini katika hayo yote naweza kuwa na furaha sana kwamba hatukuwahi kuyumba katika mamlaka yetu na walinda amani waliendelea, bila kuleta matatizo yao ya kibinafsi, yanayoathiri kazi yao na tulitekeleza wajibu ambao tumetumwa hapa na Baraza la Usalama." Anasema Tinakar

Kamanda Tinaikar akifahamika pia kwa sifa yake ya utetezi wa usawa wa kijinsia hapo ndipo anapomwaga sifa kwa wanawake ambao walikuwa wanahudumu katika kikosi chini yake akisema, "walinda amani wetu wanawake wanafanya kazi ya ajabu katika mazingira magumu sana, mara nyingi bila kitu chochote ambacho kinapaswa kuwepo kwa ajili yao.  Lakini bado wanajitolea kufanya kazi ngumu na kusonga bega kwa bega na walinda amani wa kiume, na kimsingi wafanya mengi zaidi.” 

Anapohitimisha ziara yake ya kazi katika UNMISS, Luteni Jenerali Tinaikar pia atastaafu katika jeshi la India. Anasema anashukuru kwa fursa hiyo ya kuweza kuhudumu katika kutetea nchi yake na watu kote ulimwenguni kwa miaka 42. 

 

Audio Credit
Leah Mushi/John Kibego
Sauti
2'31"
Photo Credit
UNMISS/Video Still