Mzozo huu umesababisha raia wengi katika eneo la Ukanda wa Gaza kupoteza makazi yao ambayo yameshambuliwa na kusambaratishwa kabisa na mabomu yanayo poromoshwa na Israel. Katika picha mwanamke analia kwa uchungu baada ya kurejea katika makazi yake na kukuta ni kifusi tu baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa serikali ya Israel, IDF.
Wananachi wengi wa Ukanda wa Gaza wamekimbia makazi yao na kusaka hifadhi katika maeneo mengine baada ya nyumba zao kushambuliwa na wanajeshi wa IDF kuwaamuru kuondoka kkutoka maeneo hayo. Pichani watoto wameketi juu ya mitungi huku wakisubiri kuchota maji katika mfreji ulioko nje ya shule wanamoishi inayofadhiliwa na UNRWA.
Tangu kuanza kwa mzozo huko Gaza upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo huduma za mawasiliano na umeme imekuwa ni changamoto. Kutokana na kuishi katika kambi za wakimbizi na maeneo yasiyo kambi rasmi watu wengi wanalazimika kusaka njia mbalimbali za kupata mawasiliano na kuchaji simu ili waweze kuwasiliana na wapendwa wao walioko ndani na nje ya Gaza.
Kutokana na mzozo unaoendelea katika ukanda wa Gaza wananchi wengi wameshindwa kufanya kazi zao za kuwapatia vipato na misaada ya kiutu imekuwa ndio tegemo kubwa kwa wananchi hao. Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wadau wao wamekuwa wakipeleka misaada Gaza japo uingizaji wa misaada umekuwa wa kasi ndogo na kiwango kinachoingia ni kidogo ililinganishwa na mahitaji ya kibinadamu.
Wananchi wa Palestina wakiondoka katika eneo la kaskazini mwa Gaza baada ya kupokea amri kutoka IDF kuwa wahamie katika eneo la kusini mwa Gaza kwani walikuwa wakijiandaa kutelekeza mashambulizi makali kaskazini. Hata hivyo hata baada ya kuhamia eneo la kusini mwa Gaza wananchi hao waliendelea kuathirika na mashambulizi yaliyokuwa yakitekelezwa na IDF.
Tangu kuanza kwa mashambulizi huko ukanda wa Gaza wafanyakazi 146 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA wamepoteza maisha mpaka sasa. Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa tarehe 13 Novemba 2023 duniani kote walipeperusha bendera nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliopoteza maisha. Kupata picha kamili bofya hapa.