Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya UNODC: Licha ya juhudi kubwa, ujangili wa wanyamapori bado unaendelea

Kundi la tembo likielekea kunywa maji kwenye kambi ya utalii Maasai Mara Kenya
Unsplash/David Clode
Kundi la tembo likielekea kunywa maji kwenye kambi ya utalii Maasai Mara Kenya

Ripoti ya UNODC: Licha ya juhudi kubwa, ujangili wa wanyamapori bado unaendelea

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Licha ya juhudi zinazoendelea kufanyika ulimwenguni kwa takriban miongo miwili zaidi ya aina 4,000 za wanyamapori  wenye thamani bado wanakabiliwa na ujangili  kila mwaka, hii ni kulingana na ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la dawa na uhalifu, UNODC.

Katika taarifa yake kutoka Vienna Austria hii leo Mkurugenzi Mkuu wa UNODC, Ghada Waly amesema kuwa "Uhalifu dhidi ya wanyamapori una madhara makubwa kwa mazingira pia, unahatarisha riziki, afya ya umma, utawala bora, na uwezo wa dunia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi" . 

Ripoti ya Uhalifu wa Wanyamapori Duniani ya shirika hilo inachunguza juhudi za kupambana na ujangili ulimwenguni kote.

Ingawa kuna ishara chanya kwamba kupambana na ujangili wa baadhi ya aina za wanyamapori maarufu ambao unaonesha umepungua, ikiwa ni pamoja na tembo na kifaru - kwa sababu ya kuvunjwa kwa mitandao ya ujangili  na kukandamiza mahitaji katika masoko makuu - taswira kamili kwa maelfu ya mimea na wanyama walio hatarini bado inasikitisha.

Upeo na madhara

Kwa mujibu wa UNODC, uhalifu dhidi ya wanyamapori una athari kubwa kimataifa na mara nyingi, madhara sio bayana. 

Takwimu za hivi karibuni kuhusu aina za wanyama na mimea zilizonaswa wakati wakati wa ujangili kuanzia mwaka 2015 hadi 2021 katika nchi 162 na maeneo mengine zinaonesha kuwa biashara haramu inaathiri karibu aina 4,000 za mimea na wanyama, ambapo takriba aina 3,250 zimeorodheshwa chini ya Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Aina za Wanyamapori na Mimea Iliyohatarishwa (CITES). 

Wakati ripoti hii ilipokuwa ikitolewa, mashirika ya utekelezaji wa sheria yalikamata bidhaa milioni 13 zilizokuwa tani 16,000 kwa jumla. 

Licha mchango wake mkubwa katika kutoweka kwa nyingi ya aina ya mimea ana wanyampori adimu, kama vile orchid, mimea inayoweza kuhifadhi maji, reptilia, samaki, ndege, na mamalia, ujangili wa wanyamapori mara nyingi haupewi kipaumbele na umma, kulingana na wataalamu wa UN katika kuzuia uhalifu wa wanyamapori. 

Kwa mfano, hivi karibuni ukusanyaji haramu kwa ajili ya biashara unadhaniwa kusababisha kutoweka kwa aina kadhaa za mimea inayoweza kuhifadhi maji zilizo kusini mwa Afrika. Pia imeleta upungufu mkubwa wa orchid adimu, ikiwa aina zilizogunduliwa hivi karibuni ndizo hulengwa haraka na wawindaji na wanunuzi haramu.

Athari kwa mazingira na mabadilik ya tabianchi yatokanayo na usafirishaji haramu wa wanyama pori
UNODC/ Ripoti ya dunia ya uhalifuwa wa wanayamapori
Athari kwa mazingira na mabadilik ya tabianchi yatokanayo na usafirishaji haramu wa wanyama pori

Madhara kwa mazingira na tabianchi yanayosababishwa na biashara haramu ya wanyamapori.

Mbali na kutishia idadi ya aina za wanyamapori moja kwa moja, ujangili wa wanyamapori unaweza kuvuruga mifumo dhaifu ya ekolojia na majukumu yake, hasa kudhoofisha uwezo wake wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Isitoshe, wataalamu katika afya ya binadamu na wanyama wameonya mara kwa mara kuhusu hatari za magonjwa yanayohusiana na biashara ya wanyamapori katika miongo ya hivi karibuni. 

Tahadhari hizi ni pamoja na usambazaji wa moja kwa moja wa magonjwa kwa binadamu kutoka kwa wanyama walio hai, mimea na bidhaa za wanyamapori ikiwa ni pamoja na nyama ya porini, na hatari zinginezo kwa sababisha upungufu wa idadi ya wanyamapori, mifumo ya ekolojia na uzalishaji wa chakula.

Adui mkuu

Uchambuzi wa zaidi minaso 140,000 ya aina za wanyamapori waliolanguliwa tangu 2015 hadi 2021 unadhihirisha kwamba vikundi sugu vya uhalifu wa kupangwa vinaharibu mifumo ya ekolojia iliyo hatarini duniani kote, kutoka misitu ya Amazon hadi Golden Triangle (kwa ujumla, ikijumuisha kaskazini-mashariki mwa Myanmar, kaskazini-magharibi mwa Thailand na kaskazini mwa Laos). 

Mitandao ya uhalifu ya kimataifa inashiriki katika hatua mbalimbali na kwa namna tofauti tofauti, ikiwa ni pamoja na usafirishaji, uingizaji, udalali, uhifadhi, uzalishaji na uuzaji kwa wateja.

Kifaru mama na mwanaye wakiwa wamelala kivulini kwenye ziwa Rhine na hifadhi ya wanyapori nchini Uganda
© UNDP/Gregoire Dubois
Kifaru mama na mwanaye wakiwa wamelala kivulini kwenye ziwa Rhine na hifadhi ya wanyapori nchini Uganda

Mara kwa mara,walanguzi hubadilisha mbinu na njia za kuepuka kugunduliwa na kushtakiwa, kwa kutumia mapengo ya kisheria na udhaifu katika utekelezaji, kwa mujibu wa UNODC. Ufisadi huzidisha madhila dhidi ya wanyama na mimea, huku maafisa wakipuuza uvunjaji wa sheria. 

Licha ya hili, ni nadra sana kupata kuwa uhalifu unaohusisha wanyamapori umeshtakiwa kama kesi ya ufisadi, na hili huwapa nafasi wahalifu kuepuka adhabu. "Kukabiliana na uhalifu huu, lazima tuwe na uwezo na ujanja sawa na majangili wa wanyamapori. 

Hii inahitaji hatua madhubuti na maalum kwa pande zote za wanunuzi na wauzaji, jitihada za kupunguza motisha za uhalifu na faida kutokana na ujangili , uwekezaji mkubwa katika takwimu, uchambuzi, na uwezo wa kufuatilia," alieleza Ghada Waly.

Kuna matumaini

Uchanganuzi wa hivi karibuni wa ujangili wa tembo na vifaru umedhihirisha kuwa mkakati kamili unaoshughulikia wauzaji na wanunuzi wa bidhaa haramu umetoa matokeo mazuri. Lakini mbinu hii lazima pia iungwe mkono kwa umakini zaidi na sera, kanuni kali za kuthibiti biashara, na hatua za utekelezaji wa sheria zilizolengwa dhidi ya walanguzi sugu. 

Kumekuwa na kupungua kwa kiasi kikubwa katika ujangili, kunaswa kwa bidhaa za haramu, na bei za aina ya wanyama na mimea iliyo hatarini, katika muongo uliopita, ilibainisha UNODC.

Soma ripoti kamili