Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfanyakazi wa UN auawa huko Gaza; Guterres ataka uchunguzi kufanyika

Kuteremsha bendera ya UNRWA nusu mlingoti katika Ofisi ya UNRWA Lebanon huko Beirut.
© UNRWA/Fadi El Tayyar
Kuteremsha bendera ya UNRWA nusu mlingoti katika Ofisi ya UNRWA Lebanon huko Beirut.

Mfanyakazi wa UN auawa huko Gaza; Guterres ataka uchunguzi kufanyika

Amani na Usalama

Mfanyikazi wa Idara ya Usalama na Ulinzi ya Umoja wa Mataifa (DSS) amefariki na mwingine kujeruhiwa wakati gari lao la Umoja wa Mataifa liliposhambuliwa walipokuwa wakisafiria kwenda Hospitali ya Europe huko Rafah, Gaza hii leo Jumatatu.

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq katika taarifa yake kwa waandishi wa habari kutoka New York Marekani amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani mashambulizi yote dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na ametaka uchunguzi kamili ufanyike. 

“Huku mzozo wa Gaza ukiendelea kuathiri sana - sio tu raia, lakini pia wafanyakazi wa kibinadamu - Katibu Mkuu anasisitiza ombi lake la haraka la kusitishwa kwa mapigano kwas ababu za kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka wote," alisema.

Awali akihojiwa na waandishi wa habari, Bw. Haq alisema kuwa Umoja wa Mataifa bado unakusanya taarifa kuhusu tukio hilo.  Baadaye alithibitisha kwamba afisa wa usalama aliyeuawa alikuwa mfanyakazi wa kimataifa, na hivyo kuashiria kifo cha kwanza kama hicho cha Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Gaza.

Katika hatua nyingine, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA liliripoti kuwa mfanyakazi wake mwingine ameuawa katika vita hivyo na kufanya idadi hiyo kufikia 188.

Afisa huyo mkuu wa miradi mwenye umri wa miaka 53 aliaminika kufariki katika shambulio lililotekelezwa na Israel katika mji wa kati wa Deir Al Balah, baada ya kuondoka Rafah.