Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Tamu chungu’ kwa watu wa asili zawekwa bayana kwenye IW2024

Muonekano wa mshiriki wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 23 cha Jukwaa la Kudumu la Masuala ya Wenyeji.
UN Photo/Manuel Elías
Muonekano wa mshiriki wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 23 cha Jukwaa la Kudumu la Masuala ya Wenyeji.

‘Tamu chungu’ kwa watu wa asili zawekwa bayana kwenye IW2024

Haki za binadamu

Mkutano wa 23 wa Jukwaa la Kudumu kuhusu Masuala ya Watu wa Asili, UNPFII likiwa leo limeingia siku ya nne kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, miongoni mwa mambo yaliyofanyika ni uzinduzi wa kitabu cha mwaka huu wa 2024 kuhusu watu wa asili kikipatiwa jina Dunia ya Watu wa asili, au IW2024, kikiwa ni toleo la 38.

Kitabu hicho hutolewa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kinamulika kwakina haki za watu wa asili kwenye ardhi, maeneo  na rasilimali zao.

Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili, UNDRIP la mwaka 2007, limetenga ibara zake nyingi kuhusu haki za ardhi, kwa kutambua kuwa hiyo ni haki ya msingi ya kibinadamu kwa watu wa asili.

Toribia Lero Quispe, mtetezi wa haki za binadamu kutoka Bolivia akiwa kwenye uzinduzi wa IW2024.
UN Video
Toribia Lero Quispe, mtetezi wa haki za binadamu kutoka Bolivia akiwa kwenye uzinduzi wa IW2024.

Mafanikio na changamoto

Kupitia toleo la mwaka huu la kitabu hicho, lenye kurasa 688, watu wa asili kutoka Afrika, Asia, Amerika, Karibea, Pasifiki na Ulaya wamemulikwa hususan fursa chanya zilizojitokeza halikadhalika changamoto zao kuhusu umiliki wa ardhi, maeneo yao na rasilimali umewekwa bayana.

Mathalani nchini Cameroon, ingawa haijaridhia UNDRIP, imefanya mabadiliko ya kisheria kuhakikisha kwamba watu wa asili wanapewa wajibu wa kusimamia na kufuatiali miradi mikubwa kama vile mabwawa, barabara na madini ambayo inatekelezwa kwenye maeneo yao.

Mbilikimo DRC wakumbwa na changamoto

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, nako mwaka 2022 kulipitishwa sheria ya kulinda na kusongesha haki za watu zaidi ya milioni 1.2  wa jamii ya asili wanaoishi misituni, sheria iliyoanza rasmi kutumika mwaka 2023 ambapo serikali kwa kusaidiana na mashirika ya kiraia wanatekeleza kanuni za uhifadhi wa misitu unaohusisha watu hao wa asili.

Watu hao wa asili nchini DRC wametapakaa katika majimbo yote 26 ya taifa hilo la Maziwa Makuu ambapo IW2024 inasema mapigano mashariki mwa nchi yanaathiri maisha ya watu wa asili.

“Mwaka 2023, utapiamlo na ukosefu wa huduma bora za afya ulisababisha vifo vya zaidi ya viongozi 20 wa jamii hiyo kwenye kambi ya Karanyuchinya pekee, sambamba na watoto mbilikimo 43 na wanawake 23,” kimesema kitabu hicho kikitanabaisha kuwa, “matokeo yake, mbilikimo hao wananyimwa haki yao ya kutekeleza maarifa yao ya asili, kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.”

Waliotoka Rutshuru na maeneo ya Nyiragongo jimboni Kivu Kaskazini hawakuwa wamesajiliwa hivyo walinyimwa haki yao ya kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa 2023, kimesema kitabu hicho.

Edward Porokwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wafugaji na Watu wa Asili, PINGO nchini Tanzania.
UN Video
Edward Porokwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wafugaji na Watu wa Asili, PINGO nchini Tanzania.

Uhifadhi na haki za watu wa asili

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho, Edward Porokwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wafugaji na Watu wa Asili, PINGO nchini Tanzania amesema hoja ya uhifadhi wa maeneo imekuwa ‘mwiba’ kwa watu wa asili.

“Tunavyozungumza sasa Tanzania ni bingwa wa uhifadhi ambapo zaidi ya asilimia 45 ya eneo la nchi ni maeneo ya hifadhi. Je hii ina maana gani kwa watu wa asili? Ina maana kuendelea kwa uwepo wao? Ina maana kupoteza mbinu za wao kuishi?” aliuliza Bwana Porokwa.

Mahakama ya Haki Afrika nayo yatajwa

Nchini Uganda, kwa minajili ya uhifadhi, Mamlaka ya Uhifadhi ya Uganda mwaka jana ilifurusha watu wa jamii ya Benet na kuchoma moto nyumba 95 na kuwakamata wengine 70, imesema IW2024, ambapo hadi sasa licha ya suala hilo kufikishwa mbele ya Mahakama ya Haki za binadamu ya Afrika, ACHPR, bado hakuna hatua iliyochukuliwa.

Huko Kenya, mapema mwezi Novemba, mamlaka kutoka shirika la Kenya la uhifadhi wa wanyamapori, walifurusha watu 700 wa kabila la Ogiek, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto. Tukio lilifanyika siku chache tu kabla ya kufurushwa.

Kitabu kinasema kitendo cha serikali kilikuwa kinyume na uamuzi wa ACHPR unaotambua umiliki wa kabila la Ogiek kwenye ardhi yao ya asili katika msitu wa Mau.

Hata hivyo kitabu kinatambua hatua kubwa zilizopigwa hadi sasa na watu wa jamii ya asili katika utetezi wa haki zao sambamba na ushirikiano wao na serikali.

Soma kitabu kizima hapa.