Shirika la UM juu ya Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba katika mwaka huu pekee Wasomali 22,000 walihatarisha maisha walipojaribu kuvuka Ghuba ya Aden, kutokea Usomali na kuelekea Yemen, kwa kutumia mashua zilizoregarega na zisiokuwa imara.
Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) wiki hii limewakilisha rasmi mchezo mpya wa kompyuta, kwa lugha ya Kiswahili, unaopatikana kwenye mtandao, uliokusudiwa kutumiwa na vijana ili kuwasaidia kwenye zile juhudi za kujifunza mfumo unaoridhisha wa maisha ili, hatimaye, wafanikiwe kujikinga na hatari ya maambukizo ya virusi maututi vya UKIMWI. ~~
Wiki hii Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio la kuongeza kwa miezi sita zaidi opereshani za UM za juu ya ulinzi wa amani katika Sahara ya Magharibi zinazoongozwa na Shirika la MINURSO. Operesheni hizi zinatarjiwa kuendelea hadi mwezi Aprili 2007.
Ripoti ya KM, iliyowasilishwa wiki hii kuhusu hali katika Sahara ya Magharibi imependekeza Baraza la Usalama kutoa mwito kwa Morocco na Chama cha Ukombozi wa Sahara ya Magharibi, Frente Polisario, wa kuwahimiza kushirki kwenye majadiliano yasio na shuruti, ya kutafuta suluhu ya kuridhisha na ya kudumu, itakayowawezesha wazalendo wa Sahara ya Magharibi hatimaye kutekelezewa haki ya kujiamulia wenyewe utawala halali.
Ripoti ya tano juu ya haki za kiutu ya Shirika la Ulinzi wa Amani katika Liberia (UNMIL) imeonya ya kuwa makosa ya jinai ya kijinsia, ya kutumia nguvu na mabavu dhidi ya wanawake na watoto wadogo bado yanaendelea kuendelezwa katika Liberia.
Mapema wiki hii, KM Kofi Annan aliwasilisha mbele ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu, ambayo inahusika na masuala ya kijamii, kiutu na kitamaduni, ripoti maalumu inayozingatia tatizo sugu, na karaha, la utumiaji nguvu dhidi ya wanawake.
Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, Ibrahim Gambari wiki hii anzuru Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa madhumuni ya kuhakikisha uchaguzi utakaofanyika nchini mwisho wa mwezi kuchagua raisi na pia wawakilishi wa baraza la majimbo utakuwa wa amani.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bwana Willam Lacy Swing ameeleza wasi wasi mkubwa kutokana na kutangazwa maneno ya chuki dhidi ya wazungu kwenye vyombo vya habari.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limelaani vikali sana habari za kutokea vitendo zaidi vya ubakaji huko Zimbabwe na likihimiza sheria mpya kupitishwa kuwalinda watoto wa nchi hiyo na kutoa masomo zaidi juu ya virusi vua HIV na Ukimwi.
Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limepokea msaada wa yuro milioni 105 kutoka Kamisheni ya Ulaya zitakazotumiwa kusaidia huduma za kugawa chakula kwa umma muhitaji wa kimataifa katika 2006.