Makala za wiki

Mawaziri wanazingatia msukumo mpya kugharamia maendeleo

Mkutano wa Hadhi ya Juu ulifanyika kwenye Makao Makuu mjini New York kusailia hatua za kuchukuliwa kukamilisha maafikiano yaliopitishwa mwaka 2000 kwenye mji wa Monterrey, Mexico. Maafikiano ya Monterrey hasa yalidhamiria kuongeza ushirikiano wa kiuchumi wenye nguvu, na ulio bora, kwa umma wa kimataifa ili kupiga vita umasikini. Maafikiano ya Monterrey yalipendekeza kuzingatiwe masuala yanayoambatana na usimamizi wa kizalendo wa gharama za kuhudumia maendeleo; na kusailia taratibu madhubuti za ugawaji wa misaada ya kimataifa. ~~Sikiliza ripoti kamili kwenye idhaa ya mtandao.

Mkutano muhimu wafanyika London kuzuia vifo vya mama wazazi

Taarifa za UM zimeripoti kwamba wajumbe zaidi ya 1,800 wanaohusika na maandalizi ya sera za kitaifa, pamoja na wataalamu, wawakilishi wa mashirika yasio ya kiserekali (NGOs), wanaharakati wanaogombania haki za wanawake na vile vile watu mashuhuri kadha wa kadha kutoka nchi 100 ziada walikusanyika karibuni mjini London kwenye mkutano maalumu ulioahidi kulipa “umuhimu, wa kiwango cha juu, suala la kuboresha afya ya mama wazazi." Kadhalika wajumbe hawo waliahidi kuliingiza suala la kuboresha huduma za uzazi kwenye ajenda za miradi ya afya, kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mkurugenzi wa UNDP asifu maendeleo ya uchumi Afrika kusini ya Sahara

Kemal Dervis, Mkurugenzi Msimamizi wa UNDP karibuni alifanya ziara ya siku 10 katika Msumbiji, Rwanda na Tanzania. Aliporejea Makao Makuu aliitisha mkutano na wanahabari wa kimataifa katika mwanzo wa wiki na alielezea kwamba ule mfumo wa kuambatanisha utekelezaji wa miradi ya mashirika ya UM chini ya mwongozo mmoja, kitaifa, unatekelezwa kwa taratiibu zenye kutia moyo sana katika zile nchi alizozitembelea.

KM anakhofia athari zisioridhisha baada ya SPLM kukata ushirikiano na Serikali ya Muungano

Kundi la SPLM la Sudan Kusini limetangaza mwanzo wa wiki kujitoa kutoka Serikali ya Muungano na Chama Tawala cha NCP na kuzusha mzozo wa kisiasa ndani ya nchi.

Juhudi za UM kuboresha huduma za maendeleo Tanzania

Kemal Dervis, Mkurugenzi Msimamizi wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) wiki hii alianza ziara ya siku 10 katika bara la Afrika kwa madhumuni ya kufufua tena zile juhudi za kuyakamilisha Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati, hususan katika zile nchi ambazo bado zinazorota na kuwachwa nyuma katika kuitekeleza miradi ya kupunguza umaskini kwa nusu katika 2015.

Kamati za Baraza Kuu zaanza kujadilia ajenda za kikao cha 62

Baraza Kuu la UM lina kamati sita ambazo zimegaiwa majukumu kadha wa kadha yanayohusiana na masuala ya kimataifa yenye kuhitajia suluhu ya kipamoja miongoni mwa jamii ya kimataifa.

Walimwengu watambua mchango wa watu wazee katika maendeleo

Tarehe 01 Oktoba iliadhimishwa na UM kuwa ni ‘Siku Kuu ya Watu Wenye Umri Mrefu/Watu Wazee’ na kulitolewa mwito maalumu ulioyahimiza mataifa yote wanachama kuandaa miradi ya kizalendo, kwa dhamira ya kuwapatia umma wa kimataifa wenye umri wa miaka 60 na zaidi, wanaotafsiriwa kama watu wazee, pensheni ya kudumu maridhawa itakayowasaidia kuishi vizuri kama raia wengine wenziwao.

Baraza Kuu lakhitimisha mjadala wa mwaka na kuhimiza kuwepo vitendo badala ya maneno

Mjadala wa kikao cha 62 cha wawakilishi wote ulioshtadi katika ukumbi wa Baraza Kuu, mjini New York, kuanzia tarehe 25 Septemba, ulikamilishwa na kutiwa kikomo Ijumatano tarehe 03 Oktoba. Kabla ya mijadala kuanza wajumbe kutoka nchi 191 wanachama walitatarajiwa kuwasilisha sera zao kuhusu uhusiano wa kimataifa. Baada ya mijadala kukamilishwa wawakilishi kutoka mataifa 189 ndio waliosajiliwa kumudu kuzungumzia kikao.