Makala za wiki

Ziara ya NKM Asha-Rose Migirio Austria kuhutubia Kikao cha Kuhuisha Serekali

Naibu KM Asha-Rose Migiro Ijumanne alihutubia Kikao cha Saba cha Kimataifa kilichojumuika kwenye mji wa Vienna, Austria kuzingatia taratibu za kurudisha hali ya kuaminiana kati ya wenye madaraka wenye kuendesha serekali na raia wanaotawaliwa.

Juhudi za kimataifa kupiga vita utekaji nyara wa watoto Afrika

Majuzi wawakilishi wa mataifa zaidi ya 10 kutoka Afrika Mashariki na eneo la Maziwa Makuu walikusanyika mjini Kampala, Uganda kwenye mkutano wa Shirika la UM dhidi ya Jinai na Madawa ya Kulevya (UNODC), na walizingatia ratiba ya sheria imara dhidi ya biashara ya magendo ya kuteka nyara watu na watoto, na kuwavusha mipaka kutoka makwao na kuwapeleka kwenye maeneo mengineyo kuendeleza ajira haramu, ya lazima, inayotengua kabisa haki za kibinadamu.~~

Hali ya uchumi na jamii duniani kwa 2007

Ripoti ya UM juu ya Uchunguzi wa Hali ya Uchumi na Jamii Duniani kwa 2007 ilioelezewa kwa muktadha usemao \'Maendeleo katika Dunia yenye Kuzeeka\' iliwakilishwa wiki hii mbele ya waandishi habari wa kimataifa na Jose Antonio Ocampo, Makamu KM anayehusika na masuala ya uchumi na jamii. Ripoti iliashiria ya kuwa watu milioni 1.2 wenye umri wa miaka 60 na zaidi, watakuwa wanaishi kwenye mazingira ya hali iliokosa kile kinachojulikana kama ‘wavu wa hifadhi ya jamii’. Asilimia 80 ya fungu hili la umma wa kimataifa litakutikana zaidi katika mataifa yanayoendelea.

Siku ya Kuwakumbuka Wahamiaji Duniani

Ijumatano ya tarehe 20 Juni mwaka huu iliadhimishwa katika sehemu kadha wa kadha za ulimwengu kuwa ni ‘Siku ya Wahamiaji Duniani’, kumbukumbu zilizoshika fora katika kipindi ambapo pia kulitolewa mwito muhimu unaohimiza jumuiya ya kimataifa kukuza ushirikiano wao katika kuwasaidia wenziwao waliofurushwa makwao na kunyimwa makazi na maskani. Kadhalika mnamo siku hiyo kuliwasilishwa onyo lenye kuhadharisha walimwengu ya kwamba idadi ya wahamaji huenda kuongezeka katika kipindi kijacho.

Sudan yakubali vikosi vya mseto vya kimataifa kwa Darfur

Baada ya kufanyika mashauriano ya kiufundi, ya siku mbili, kwenye mji wa Addis Ababa, Ethiopia katika wiki hii, kati ya wawakilishi wa UM na wale wa kutoka AU, pamoja na wajumbe wa Serekali ya Sudan, kulidhihirika fafanuzi za kuridhisha juu ya yale masuala yaliokuwa yakikwamisha utekelezaji wa mpango wa kupeleka vikosi vya mseto kulinda amani katika jimbo la magharibi la Darfur. Baada ya kikao cha Addis Ababa kulitolewa taarifa ya pamoja kati ya Serekali ya Sudan na AU iliosema ya kuwa Sudan imeridhia na kuidhinisha ule mpango wa kupeleka vikosi vya mseto vya UM na AU kwenye jimbo la Darfur.

Biashara za vijijini Afrika zitafaidika na mfuko mpya wa UM

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) lilitangaza majuzi mjini Cape Town, Afrika Kusini kwenye mkutano wa Athari za Uchumi wa Dunia kwa Afrika, ya kwamba litaanzisha taasisi mpya ya mfuko wa maendeleo kusaidia wanavijiji masikini katika Afrika, kupata fedha za kuanzisha aina mpya ya biashara kwenye maeneo yao.

Naibu KM aonya "Afrika imepwelewa kutekeleza MDGs"

Naibu KM Asha-Rose Migiro aliwasilisha ripoti mpya ya UM kuhusu maendeleo katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)katika mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara. Alionya ya kuwa juhudi za kuyakamilisha malengo hayo kwa wakati ziko nyuma na zinazorota.

Jamii ya kimataifa yaadhimisha 'Siku ya Mazingira Duniani'

Tarehe 05 Juni huadhimishwa kila mwaka kuwa ni \'Siku ya Mazingira Duniani\'. Sherehe aina kwa aina hufanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa yaliopo New York na katika sehemu nyengine za ulimwengu ambapo UM huendeleza shughuli zake.~

Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Walinzi wa Amani Duniani

Tangu miaka mitano iliopita, UM uliweka kando tarehe 29 Mei kuwa ni siku ya kuadhimishwa rasmi mchango wa wafanyakazi wa kimataifa, waume na wake, wa kutoka kanda mbalimbali za dunia ambao walitumia ujuzi wao, chini ya bendera ya UM, kulinda na kuimarisha amani ya kimataifa, na kuwapunguzia mateso ya hali duni umma wa kimataifa, pamoja na kuendeleza haki za binadamu na kudumisha huduma za maendeleo katika sehemu kadha wa kadha za ulimwengu.