Hapa na pale

Hapa na Pale

Raisi mstaafu wa Marekani Bill Clinton, Ijumatatu, tarehe 06 Julai atafanya ziara ya awali katika Haiti, kama Mjumbe Maalumu wa KM kwa taifa hilo. Atakapokuwepo Haiti atakutana kwa mashauriano na maofisa wa Serikali juu ya namna ya kulisaidia taifa kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana na matatizo ya vimbunga, kuzalisha ajira mpya na kuimarisha huduma za kimsingi za jamii. Clinton pia atajadilia taratibu za kufungamanisha shughuli za UM, jumuiya za kiraia na jamii ya wafadhili wa misaada ya maendeleo na miradi ya Serikali katika kufufua huduma za uchumi na jamii.

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ambaye yupo Ujapani kwa hivi sasa, Ijumatano alikutana kwa mazungumzo na viongozi wa taifa hilo, ikijumlisha Waziri Mkuu Taro Aso, na walisailia mwelekeo wa kufuatwa na jumuiya ya kimataifa ili "kukamilisha makubaliano yanayoridhisha" kwenye mkutano ujao wa Copenhagen juu ya udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Vile vile walishauriana juu ya masuala yanayoambatana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK), Myanmar, mchango wa Ujapani katika kuendesha shughuli mbalimbali za UM, hasa katika operesheni za kulinda amani, na pia kuzungumzia taratibu za kufuatwa na wafanya biashara zitakazohakikisha kunakuwepo maendeleo yanayosarifika. Alkhamisi KM ataelekea Singapore kabla ya kwenda Myanmar Ijumaa.

Hapa na pale

Vikosi vya Uangalizi vya UM katika Georgia (UNOMIG) vimesitisha rasmi shughuli zao kuanzia tarehe 16 Juni 2009, baada ya Baraza la Usalama liliposhindwa kupitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni hizo. Wanajeshi wa UNOMIG wameshaanza kuondoka Georgia kwa hivi sasa. Taarifa ya KM iliyashukuru makundi husika kwa ushirikiano wao na vikosi vya UNOMIG tangu pale vilipoanza operesheni zake katika 1993. KM alisema UM upo tayari kutumika kwenye shughuli nyenginezo za kuimarisha amani katika Georgia. Kwa kulingana na pendekzo hilo KM amemtaka Mjumbe Maalumu wake anayehusika na UNOMIG, Johan Verbeke kuendelea kuiwakilisha UM kwenye majadiliano ya Geneva yanayozingatia usalama na ututlivu wa eneo husika, mazungumzo yanayozingatia pia suala la kuwarudisha makwao wahamiaji waliopo nje na wale wa ndani ya nchi.

Hapa na pale

KM anatarajiwa kuzuru rasmi Myanmar kuanzia tarehe 03 - 04 Julai, kwa kuitika ombi la Serikali. Atakapokuwepo huko atakutana, kwa mashauriano ya ana kwa ana, na viongozi wakuu wa Serikali ambapo wanatarajiwa kuzungumzia masuala kadha yenye umuhimu kwa UM na jamii ya kimataifa. Alitilia mkazo kwenye mazungumzo yao mambo matatu yatapewa umuhimu wa hadhi ya juu, kwa kulingana na hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa hivi sasa. Masuala hayo yanahusu, awali, kuachiwa wafungwa wote wa kisiasa, ikijumlisha Daw Aung Suu Kyi; kurudisha mazungumzo ya upatanishi kati ya Serikali na Wapinzani; na kusailia maandalizi ya uchaguzi wa taifa ulio huru na wa haki.

Hapa na pale

KM alikutana na viongozi wa kundi la Wapatanishi wa Pande Nne juu ya Mashariki ya Kati kwenye mji wa Trieste, Utaliana na walizingatia masuala matano muhimu: mwelekeo unaofaa kuchukuliwa kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na Falastina; kuwasaidia wenye mamlaka wa KiFalastina (PA) kutawala bora kwenye maeneo yao na kukuza uchumi; hali katika Tarafa ya Ghaza; suala la kuleta amani kamili kati ya Israel na Syria, na Israel na Lebanon; na kusailia Mkutano Mkuu wa Moscow utakaofanyika baadaye kutathminia uwezekano wa kurudisha amani katika Mashariki ya Kati.