UNFPA na Taasisi ya Panzi DRC yaingia makubaliano kunusuru manusura wa ukatili wa kingono
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yamekuwa mwiba siyo tu katika usalama wa taifa hilo bali pia kwa wanawake na wasichana ambao hukumbwa na ukatili wa kingono kule kwenye mapigano. Mashirika ya kiraia yamekuwa yakiunga mkono harakati za Umoja wa Mataifa za kuhakikisha manusura wa ukatili huo wanarejeshewa siyo tu utu lakini pia kujiamini na kuendelea na maisha. Miongoni mwa mashirika hayo ni taasisi ya hospitali ya Panzi inayoongozwa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Dokta Denis Mukwege.