Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEP: Dunia haijajiandaa, fedha za kukabili mabadiliko ya tabianchi hazitoshi huku joto likitarajiwa kuvuka nyuzi joto 1.5

Watu wanapanda mti mmoja uliozungukwa na maji kando ya ufuo huko Chattogram, Bangladesh, huku maji yanayopanda yakifunika pwani.
© WMO/Kazi Md Jahirul Islam Watu wanapanda mti wa mwisho uliosimama huku maji yanayopanda yakifunika ufuo huko Chittagong, Bangladesh.

UNEP: Dunia haijajiandaa, fedha za kukabili mabadiliko ya tabianchi hazitoshi huku joto likitarajiwa kuvuka nyuzi joto 1.5

Tabianchi na mazingira
  • Mahitaji: Nchi zinazoendelea zitahitaji dola bilioni 305 kila mwaka kufikia 2035.
  • Ufadhili: Hata ukiongezwa mara tatu, utatosheleza asilimia 29 tu ya mahitaji.
  • Onyo la UNEP: Dunia haijajiandaa kukabiliana na ongezeko la joto kuvuka nyuzi joto 1.5.
  • Wito: Nchi ziongeze ufadhili na kuharakisha hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Wakati ongezeko la joto duniani likitarajiwa kuvuka nyuzi joto 1.5, ufadhili wa kusaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bado hautoshi kukidhi mahitaji, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) katika ripoti iliyochapishwa leo Jumatano.

Ripoti hiyo ya 2026 kuhusu “Pengo la Utekelezaji wa Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” (Adaptation Gap Report 2026) imebaini kuwa nchi zinazoendelea zitahitaji takribani dola bilioni 305 kila mwaka ifikapo mwaka 2035 ili kujenga uwezo wa kustahimili athari za tabianchi na kupunguza hatari zake.

Hata hivyo, iwapo ufadhili wa umma wa kimataifa kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi utaongezwa mara tatu, kiwango cha juu kitakachoweza kugharamiwa ni asilimia 29 tu ya mahitaji hayo.

“Dunia haijajiandaa kukabiliana na hali ya sasa ya tabianchi, achilia mbali athari zitakazotokana na ongezeko la joto duniani kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5,” ameonya Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.

Ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unapungua

Ripoti hiyo imechapishwa kabla ya mkutano wa  wa Umoja wa Mtaifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP31, unaotarajiwa kuanza wiki ijayo mjini Antalya, nchini Uturuki.

Ripoti imebaini kuwa:

  • Juhudi za kimataifa za kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bado hazina ufadhili wa kutosha.
  • Vikwazo vya kitaasisi vinakwamisha utekelezaji wa hatua zinazohitajika.
  • Wakati huohuo, hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuongezeka.

Ufadhili wa umma wa kimataifa kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ulifikia kati ya dola bilioni 28.2 na bilioni 31.7 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la takribani dola bilioni moja tu ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Ongezeko la ufadhili huo linaanza kudorora. Aidha, makadirio ya dola bilioni 305 hayajajumuisha mahitaji ya sekta binafsi, hali inayomaanisha kuwa kiasi hicho kinaweza kuongezeka mara mbili.

Juhudi zaidi zahitajika

Wito wa kuongeza mara tatu ufadhili wa kila mwaka ulikubaliwa katika mkutano wa mwaka jana wa mabadiliko ya tabianchi nchini Brazil na ni sehemu ya matokeo muhimu ya mkutano huo yaliyopewa jina la Global Mutirão. Neno Mutirão ni la Kireno, likitokana na lugha ya wenyeji na kumaanisha “jukumu la pamoja”.

Hata kama lengo hilo litafikiwa, ufadhili unaokadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 85 na bilioni 120 kila mwaka utatosheleza asilimia 20 hadi 29 tu ya mahitaji yanayokadiriwa, baada ya kuzingatia ongezeko la gharama za maisha.

“Katika mkutano wa COP31 kuhusu tabianchi nchini Uturuki na mikutano itakayofuata, nchi lazima zielekeze nguvu katika kuongeza juhudi za kufikia azma ya Global Mutirão ya COP30 ya kuongeza mara tatu ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2035. Hata hivyo, zinapaswa kuelewa kuwa zitahitaji kuongeza ufadhili huo zaidi ili kuokoa maisha, kuepusha hasara na uharibifu na kulinda uchumi,” amesema Bi. Andersen.

Nchi bado zina fursa ya kufikia lengo la ufadhili

Ripoti imesisitiza kuwa nchi bado zinaweza kufikia lengo la kuongeza mara mbili ufadhili kutoka viwango vya mwaka 2019 na kufikia dola bilioni 40 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Glasgow kuhusu Tabianchi wa mwaka 2021, uliopitishwa katika mkutano wa COP26 nchini Scotland.

Benki za maendeleo za kimataifa huenda ziliongeza kwa kiasi kikubwa ufadhili wake mwaka jana. Aidha,inasema ripoti mtiririko wa fedha kati ya nchi zinazoendelea pia umeongezeka, kutoka dola bilioni 3.8 mwaka 2019 hadi bilioni 9.6 mwaka 2024.

Hata hivyo, ripoti imesisitiza kuwa ufadhili pekee hautoshi na kwamba kuna haja ya kuimarisha taasisi na kuharakisha utekelezaji wa hatua zinazohitajika ili kulinda jamii zilizo katika hatari zaidi, kujenga uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na ongezeko la hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko hayo.