Umoja wa Mataifa wazindua mwongozo wa kihistoria kuhakikisha binadamu wanadhibiti matumizi ya AI mijini
Umoja wa Mataifa hii leo Novemba 4, 2026, umezindua kwa mara ya kwanza mwongozo unaojumuisha mfumo mzima wa Umoja huo, wenye lengo la kuhakikisha kuwa binadamu, badala ya mashine, wanabaki na mamlaka na uwajibikaji katika maamuzi yanayofanywa kwa kutumia Akili Mnemba (AI) kwenye huduma za umma mijini.
Mwongozo huo umezinduliwa jijini Barcelona, Hispania, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat), UNECE na mashirika mwengine pamoja na programu 19 za Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo matumizi ya AI yanazidi kuongezeka katika utoaji wa huduma za umma duniani.
Kwa sasa, AI inatumika kujibu maswali ya wananchi, kubaini barabara zinazohitaji matengenezo na kusaidia maamuzi ya kiutawala. Hata hivyo, teknolojia hiyo inaibua wasiwasi kuhusu faragha, ubaguzi, haki za binadamu na uwajibikaji.
Mwongozo huo, unaojulikana kama U4SSC Toolbox for People-Centred Smart Cities in the AI Era, unawasaidia viongozi wa miji kutambua maeneo ambayo AI inaweza kuboresha huduma, hatua za kulinda wananchi na mazingira ambayo teknolojia hiyo haipaswi kutumika.
Katibu Mkuu wa ITU, Doreen Bogdan-Martin, amesema, “Miji ya kisasa na endelevu hupimwa kwa kiwango ambacho wananchi wananufaika na teknolojia iliyobuniwa kuboresha maisha yao ya kila siku.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat, Anacláudia Rossbach, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha teknolojia hiyo inanufaisha pia wakazi wa makazi yasiyo rasmi na maeneo yenye huduma duni, huku haki za binadamu zikilindwa.
Uzinduzi huo unaambatana na maadhimisho ya miaka 10 ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa United for Smart Sustainable Cities (U4SSC), unaosaidia miji kutumia teknolojia kufanikisha maendeleo endelevu.
Soma zaidi na upate mwongozo huo.